Kufuatia maadhimisho ya wiki ya maji yaliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es salaam, Mamlaka ya Maji safi na Majitaka (Dawasa) imesema hadi sasa, imefanikiwa kutatua kero za maji kwa asilimia 70 huu mengine yakielekezwa katika idara mbalimbali za mamlaka hiyo. Kupitia dawati maalum, zaidi ya wananchi 400 walipata nafasi ya kueleza kero zao ambapo baadhi yao wametaja uvujaji wa maji, kutopata huduma hiyo nje ya mji pamoja na usomaji wa mita.
Kuhusu tatizo la wananchi wanaoishi nje ya mji kutopata huduma ya maji, taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo imebainisha kuwa Dawasa imekuwa ikiweka asilimia 35 ya mapato yake ili kutatua changamoto hiyo kwa kutekeleza miradi midogo na mikubwa ya maji jijini.
“Dawasa imedhamiria kuboresha zaidi utaratibu wa kupokea maoni kwa wateja ikiwa ni pamoja na kuwa na dawati linalohama kutoka eneo moja hadi jingine ‘Mobile customer care desk’ ili kufikia wakazi wengi na kupokea maoni mengi zaidi lengo ikiwa ni kuboresha zaidi huduma kwa wananchi tunaowahudumia”. Imesoma taarifa hiyo.
Wakati wa maadhimisho hayo, Mamlaka hiyo imeweza kuzindua miradi ya maji maeneo mbalimbali.