Majadiliano kati ya menejimenti ya kampuni ya mabasi yaendayo kasi (Udart) na viongozi wa jiji la Dar es salaam yanaendelea ili kuhamisha kituo cha mabasi hayo kutoka eneo la Jangwani na kukipeleka kwenye kituo cha mabasi yaendayo mikoani Ubungo (UBT). Meya wa jiji Isaya Mwita amesema wamefikia maamuzi hayo ili kunusuru magari hayo kuendelea kuharibika kutokana na kituo cha Jangwani kukumbwa na mafuriko mara kwa mara mvua zinaponyesha.
Hivi sasa uongozi wa Udart pamoja na viongozi wa jiji wapo kwenye majadiliano kuhusu suala hilo ili waweze kufikia muafaka. Mwita ameeleza kuwa mpango huo unaendelea kufanyiwa kazi na halmashauri ya jiji ambayo kwa sasa ipo kwenye mchakato wa kupanua Mto Msimbazi ili maji yaweze kusafiri moja kwa moja hadi baharini. Meya huyo amesema tayari fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zimeshatolewa na awamu ya kwanza ya mradi itaanzia Salender hadi Kigogo.