Naibu Waziri wa Ujenzi Elias Kwandikwa amewataka makandarasi wanaojenga barabara kuelekea kwenye mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa Stieglers Gorge kukamilisha mradi huo ifikapo Oktoba na kusisitiza hawatopewa muda wa nyongeza.Kwandikwa ametoa agizo hilo wakati akikagua barabara hizo kwa upande wa Morogoro wa Pwani ambapo amedai fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo zipo hivyo wakandarasi hao wanapaswa kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha kazi hiyo hadi kufikia 02 Oktoba mwaka huu.
“Barabara hizi zikamilike ndani ya wiki mbili hizi na serikali haitaongeza muda kwa vile wakandarasi wote wamelipwa fedha za ujenzi huu”. Amesema Naibu Waziri Kwandikwa.
Katika maelezo yake, Naibu Waziri amedai kuwa serikali inataka ujenzi wa barabara hiyo kukamilika ndani ya muda uliopangwa ili kuharakisha ujenzi wa bwawa la kufua umeme la Stieglers Gorge mara baada ya barabara hiyo kukamilika.
“Serikali imejipanga kuhakikisha uboreshaji wa barabara hizi unafanyika kwa kiwango cha ubora ili zipitike kwa ajili ya kuwezesha shughuli nyingine za mradi huu kufanyika”. Ameeleza Naibu Waziri.