Baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Mkame Mbarawa kutembelea Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ili kuangalia mwenendo wa shughuli za ufungaji skana ambazo zitatumika kukagua mizigo pamoja na kuangalia hali ya usalama bandarini, Waziri huyo ametoa siku tano kwa TPA kumpatia taarifa kamili ya mpango wa kuunganisha shughuli zao.
Prof. Mbarawa ameeleza kuwa serikali imepanga kutumia takribani Sh. 69 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa ufungaji wa skana hizo katika bandari za Dar es salaam, Mtwara na Tanga. Amefafanua kuwa skana hizo zina uwezo wa kupima mzigo ukiwa ndani ya kontena na kuangalia gari lote kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa TPA Deusdedit Kakoko amesema mamlaka hiyo ilitoa kiasi cha Dola za Marekani 33 milioni kununua mashine za kupima mizigo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli. Ufungaji wa skana hizo unatarajiwa kuongeza uwezo wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza wateja.