Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani Jafo amesema Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es salaam (DART) wameanza maandalizi ya kutekeleza awamu ya tatu ya mradi huo ambapo mabasi yatafika Gongo la Mboto, kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
Akiwasilisha mapitio na makadirio ya mapato na matumizi mwaka 2019/2020 bungeni Dodoma, Waziri Jafo ameeleza kuwa mabasi hayo yatapita barabara ya Bibi Titi na Nyerere kufika Gongo la Mboto, Kituo Kikuu cha mabasi Kariakoo Gerezani kupitia Mtaa wa Lindi, Shaurimoyo na Uhuru kupitia Buguruni hadi Tazara.
“Awamu ya nne itahusisha barabara za Bagamoyo hadi Tegeta, Bibi Titi, Ali Hassan Mwinyi na Sam Nujoma zenye urefu wa kilometa 25.9 na awamu ya tano itahusisha ujenzi wa barabara za Mandela kuanzia eneo la Ubungo kupitia Tazara, Uhasibu kuungana na barabara za Kigamboni na barabara za kuanzia Tabata Relini hadi Segerea”. Ameeleza Jafo.
Aidha, TAMISEMI imeomba Bunge kupitisha makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2019/20 ya Shilingi 6.21 trilioni.