Serikali imeanza mazungumzo na Kampuni ya China Overseas Engineering Group Company (COVEC), ambayo imeonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa daraja litakalounganisha Tanzania Bara na Zanzibar.
Naibu Waziri wa Uchukuzi Godfrey Kasekenya amesema hayo bungeni Dodoma Aprili 28, 2023 kuwa mazungumzo hayo yalianza Machi 11, 2023 na yalihusisha wataalamu kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Sekta ya Ujenzi kwa upande wa Tanzania Bara na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa upande wa Zanzibar.
Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mwantum Dau Haji aliyetaka kujua mpango wa serikali kujenga daraja hilo, Kasekenya amesema bado mazungumzo yanaendelea na serikali inakusudia kujiridhisha na teknolojia zinazotumika katika ujenzi wa madaraja makubwa kabla ya kuanza ujenzi.
Ameeleza kuwa “daraja hili litajengwa kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa utaratibu wa PPP (Public-Private Partnership).”