Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Deusdedit Kakoko amesema wamejipanga kuhudumia takribani tani 14,374,400 ikiwa ni pamoja na makontena 208,000 katika vitengo vilivyo chini ya mamlaka hiyo kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019. Kakoko amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifafanua mipango na bajeti ya mamlaka hiyo.
“Tunatarajia kukusanya mapato ya jumla ya Sh. 1,012.586 bilioni, matumizi ni Sh. 778.297 bilioni na kupata ziada ya Sh bilioni 234.289”. Amesema Mkurugenzi huyo.
Mbali na hayo, mamlaka hiyo pia inatarajia kuhudumia meli 2,736 zenye ukubwa wa (GRT) milioni 35.880 ambapo kati ya hizo meli 1,307 ni za kimataifa, 786 zikiwa za mwambao na meli 670 zitahudumiwa katika bandari za maziwa.
Aidha, Kakoko amedai wamejipanga kukusanya mapato kwa wakati, kuzuia upotevu wa mapato na kukusanya kwa kupitia benki huku wakizingatia matumizi ya ‘flow meters’ na skana katika kuhakikisha shehena ya mafuta na shehena kwenye kontena.
“Tumejiwekea mikakati ya kuvutia shehena kwa kuboresha huduma za mamlaka kwa kutekeleza miradi mbalimbali kwa wakati uliopangwa sambamba na kuimarisha ulinzi na usalama katika bandari za mamlaka”. Ameeleza Kakoko.