Zaidi ya Tsh milioni 60 zimetumika kujenga vizimba viwili kwa ajili ya kukabiliana na changamoto ya Mamba katika vijiji vya Kanyala na Izindabo kwenye tarafa ya Buchosa, wilayani Sengerema Mkoani Mwanza.
Haya yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula wakati akijibu swali la Mbunge wa Buchosa Eric James Shigongo ambaye alitaka kujua kuhusu mpango wa Serikali wa kuendelea kujenga uzio katika sehemu za kuchota maji ili kuzuia vifo vinavyosababishwa na mamba Buchosa.
Kitandula amejibu swali hilo kwa kubainisha kuwa Wizara hiyo imetumia takribani shilingi milioni 60 kujenga vizimba.
Ameongeza kuwa Wizara ina mikakati ya aina mbili ambapo mkakati wa kwanza ni kuvuna Mamba kwa njia ya uwindaji wa kitalii, lakini pia Wizara inapopata taarifa ya mamba wasumbufu kwenye maeneo ya wananchi wizara huwavuna mamba hao kwa ajili kuzuia maafa kwa wananchi.
Amesema Wizara inatoa rai kwa waheshimiwa wabunge kuzihimiza Halmashauri zao kutenga Fedha kwenye bajeti za Halmashauri zitakazowezesha ujenzi wa vizimba katika maeneo ya Halmashauri zao, na kwamba Wizara ipo tayari kutoa wataalam kwa ajili ya kutoa taaluma na kusimamia ujenzi wa vizimba hivyo.