Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kimataifa ya Kuendeleza Nishati ya Jua (ISA), Dkt. Ajay Mathur yenye Makao Makuu yake nchini India ambaye ameeleza nia ya ISA kuwekeza katika miradi ya umeme jua nchini.
Mazungumzo kati ya Dkt. Biteko na Dkt. Mathur yamefanyika jijini New Delhi nchini India ambapo Dkt. Biteko alishiriki Wiki ya Nishati India ambayo ilienda sambamba na mikutano mbalimbali kuhusu nishati.
“ Tunawaalika mje kuwekeza Tanzania kwani tunahitaji kuwa na miradi mingi ya umeme kutoka vyanzo tofauti ili kuweza kutosheleza mahitaji ya watu wetu na kinachotupa msukumo zaidi kwa sasa ni mpango mahsusi wa misheni 300 tuliousaini mwezi Januari 2025 ambapo Tanzania tunapaswa kupeleka umeme kwa wananchi milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030,” amesema Biteko.
Dkt. Biteko ameishukuru Taasisi ya ISA kwa kuona Tanzania kama sehemu sahihi ya uwekezaji na kueleza kuwa kazi yake ni kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na miradi mingi ya nishati ambayo italeta utoshelevu wa umeme na kuchagiza maendeleo huku akisisitiza kuwa suala la kuwa na umeme wa kutosha si la kusubiri miradi inapaswa kutekelezwa sasa.
Kuhusu miradi ya umeme Jua nchini, Dkt. Biteko amesema Tanzania imeanza kutekeleza mradi wa umeme jua wa megawati 150 wilayani Kishapu mkoani Shinyanga kwa kuanza na megawati 50 ambapo megawati 100 zitaanza kutekelezwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza.
Ameongeza kuwa, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pia limepata maeneo matatu kwa ajili ya miradi ya umeme jua ambayo ni Zuzu, Dodoma (MW 60), Mkwese, Manyoni – Singida (MW 199) na Same, Kilimanjaro (MW 50) ambapo ameishukuru ISA kwa kukubali kufanya upembuzi wa awali katika maeneo hayo.
Ili kuwezesha uwekezaji wa Taasisi hiyo nchini, Dkt. Biteko amewataka Watendaji hao kuainisha maeneo ambayo wanahitaji kuwekeza ili Wataalam waanze kuyafanyia kazi.