Home VIWANDANISHATI Tanzania yatumia wiki ya nishati India kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia

Tanzania yatumia wiki ya nishati India kunadi vitalu vya mafuta na gesi asilia

0 comment 30 views

Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) imeendelea  kuhamasisha wawekezaji mbalimbali duniani kushiriki katika Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika Bahari Kuu ya Hindi na Nchi Kavu itakayozinduliwa mwezi Machi, 2025.

Matangazo ya fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia yanaendelea kupitia Kongamano na Maonesho ya Wiki ya Nishati ya India yanayofanyika katika Jiji la New Delhi, India tukio ambalo linawashirikisha zaidi ya watu 70,000 kutoka nchi zaidi ya 50 Duniani.

Katika Banda la Tanzania kwenye Maonesho hayo washiriki wengi wamevutiwa na taarifa za kijiofizikia zinazobainisha utajiri wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia zilizopo Tanzania.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ambaye anashiriki Kongamano hilo, ametembelea banda hilo la Tanzania na kuipongeza PURA kwa kutumia majukwaa ya kitaifa na kimataifa kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.

Dkt. Biteko ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha vyanzo vyake vyote vya nishati vinaendelezwa  ili kuwa na uhakika wa nishati ya kutosha wakati wote.

Katika kuelekea kwenye duru hiyo ya Tano ya Kunadi Vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema PURA imekamilisha masuala mbalimbali ikiwemo kupata Kampuni ya Kijiofizikia  iitwayo TGS ASA  yenye utaalam wa kuchakata data za mafuta na gesi asilia ambayo pia inahusika na utangazaji wa data hizo katika masoko mbalimbali duniani .

Mhandisi Sangweni amesema kampuni hiyo itatakiwa kukusanya na kuchakata data za mitetemo katika maeneo mengine ya bahari kuu ambayo hayajafanyiwa kazi ili kuongeza taarifa na data za petroli kwa wawekezaji.

Ameongeza kuwa, PURA imeshakamilisha uandaaji wa ramani inayoonesha maeneo ambayo yatatangazwa kwenye duru ya tano  inayojumuisha vitalu 26.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter