Home VIWANDAUZALISHAJI Biteko: Sekta ya madini ni nguzo muhimu maendeleo ya nchi

Biteko: Sekta ya madini ni nguzo muhimu maendeleo ya nchi

0 comment 193 views

Sekta ya Madini imetajwa kuwa nguzo muhimu na chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia rasilimali madini iliyopo nchini.

Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko ameeleza hayo Oktoba 25, 2023 alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es salaam.

“Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi,” amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, Sekta ya Madini inafungamanishwa na Sekta nyingine za kiuchumi kama vile viwanda na kilimo ili kuzalisha bidhaa mbalimbali zinazotumia madini kama malighafi mfano mbolea, betri za magari, simu, kompyuta na bidhaa nyingine.

“Niwahakikishie kuwa, mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki zaidi.

Nafurahi kusema kuwa, hadi sasa jumla ya Kampuni tisa za Kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo madini ya nikeli, kinywe, heavy mineral sands (mchanga bahari), Rare Earth Elements, dhahabu na almasi,” amebainisha Dkt. Biteko.

Amesema Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, Wizara
itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na Serikali inapata mapato stahiki.

“Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha kuwa mchango wake unakua hadi kufikia asilimia 10 ya Pato la Taifa kufikia mwaka 2025 kama ilivyo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025. Tutashirikiana na wadau mbalimbali wa Sekta kuhakisha lengo hilo linafikiwa,” ameongeza Waziri Mavunde.

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter