Home VIWANDAUZALISHAJI Miradi ya “REGROW” Ruaha italeta watalii Kusini Dkt. Abbasi

Miradi ya “REGROW” Ruaha italeta watalii Kusini Dkt. Abbasi

0 comment 273 views

Utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW) utakuwa chachu ya kuongeza idadi kubwa ya watalii katika Hifadhi za maeneo hayo.

Hivyo watekelezaji wa miradi hiyo wametakiwa kuhakikisha wanafanya kazi kwa umakini, kwa kasi inayohitajika na kwa kiwango cha juu ili ujenzi wa miundombinu yote ikamilike kwa wakati.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akikagua utekelezaji wa mradi huo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha.

Dkt. Abbasi ameongeza kuwa mradi wa REGROW pamoja na utalii pia umekusudiwa kuinua wananchi kiuchumi kupitia uhifadhi na utalii, na kuwa kwa yeyote atakaecheza na mradi huo, ni sawa na kucheza na maisha ya Watanzania.

“Kila Mkandarasi ajue hakuna hata siku moja itakayoongezwa katika mkataba maana miradi hii mingi tunataka kuipokea mwakani ili watalii wazidi kumiminika katika maeneo haya kama ilivyo kule Kaskazini,” amesema.

Mradi wa REGROW katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, mbali ya mitambo mbalimbali mikubwa na magari ya kusimamia doria na uwekaji sawa wa miundombinu, pia unajenga viwanja viwili vya ndege, cha urefu wa kilomita 1.8 upande wa Iringa na cha km 1.2 kwa upande wa mkoa wa Mbeya pamoja na majengo ya kupokelea abiria.

Mradi pia unajenga Hosteli kwa ajili ya wanafunzi zaidi ya 140, nyumba 13 za kulala wageni, nyumba kwa ajili madereva, kituo cha utafiti, na jengo la kutolea taarifa.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter