Home VIWANDAUZALISHAJI Serikali, Benki ya Dunia wajadili ushiriki Sekta binafsi

Serikali, Benki ya Dunia wajadili ushiriki Sekta binafsi

0 comment 125 views

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Lawrence Mafuru amesema Serikali inafanya majadiliano ya kimkakati na Benki ya Dunia namna ya kuiwezesha sekta binafsi kushiriki katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Ushiriki huo ni kupitia mpango wa ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi, yaani PPP.

Ameeleza hayo jijini Dodoma baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa Benki ya Dunia ulioongozwa na Mkurugenzi Mkazi Nathan Belete, ambapo wamejadili namna bora ya utekelezaji wa sheria ya PPP pamoja na uboreshaji wa mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara nchini.

Amesema majadiliano hayo ni utekelezaji wa msisitizo na maelekezo yanayotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa sasa ni wakati wa Sekta Binafsi kushirikiana na Serikali kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.

“Serikali imeanza majadiliano ya awamu ya pili na Benki ya Dunia kuhusu msaada ambao umejielekeza kwenye sekta za miundombinu na sekta zitakazoboresha mazingira ya kufanya biashara nchini” amesema Mafuru.

Aidha, amebainisha kuwa Sheria ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) inafanyiwa marekebisho ili iweze kuwa shindani, ambayo itaweza kuvutia mitaji ya Sekta Binafsi na hatimaye kuwezesha sekta hiyo kushirikiana na Serikali katika kutekeleza miradi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Nathan Belete amesema benki hiyo imeamua kujadiliana na Tanzania kuhusu namna bora ya utekelezaji wa miradi kwa njia Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) kwa kuwa ni miongoni mwa vipaumbele vya Rais Dkt. Samia.
Belete ameahidi kuendelea kushirikiana na Tanzania kwa karibu katika kutekeleza matarajio ya maendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter