Home VIWANDAUZALISHAJI Serikali ya Tanzania yasema viwanda vinne vya uongezaji thamani madini kujengwa Dodoma

Serikali ya Tanzania yasema viwanda vinne vya uongezaji thamani madini kujengwa Dodoma

0 comment 37 views

Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema, ujenzi wa Viwanda vinne vya uchenjuaji madini ya Shaba ikiwemo kiwanda cha Shengde Precious Metal Resources Co. Limited kinachoendelea kujengwa katika eneo la Mahungu Kata ya Nala Jijini Dodoma vinatarajiwa kuwa mkombozi wa wachimbaji wadogo wa Madini ya Shaba nchini.

Waziri Mavunde amebainisha hayo Februari 16, 2025 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanda hicho na kutoa pongezi kwa Kampuni ya Shengde Precious Metal Resources Co. Limited kwa uwamuzi wa kujenga kiwanda hicho Jijini Dodoma .

Aidha, Waziri Mavunde amesema Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kwa dhati kuyaongezea thamani madini hapa hapa nchini ili kukuza ajira kwa watanzania na kuongeza Pato la Taifa ambapo amewaahidi kupatiwa ushirikiano wa kutosha kutoka Serikalini.

Pamoja na mambo mengine, Waziri wa Mavunde amewataka wamiliki wa kiwanda hicho kukamilisha ujenzi wa kiwanda hicho kwa wakati ili kiweze kuanza uzalishaji kwa lengo la kuongeza tija katika Sekta ya Madini ikiwemo kuongeza ajira kwa watanzania, kipato kwa Wamiliki na kuongeza Pato la Taifa kupitia tozo mbalimbali.

Pia, Waziri Mavunde amesema, kwa kipindi kirefu wachimbaji wa Madini ya Shaba wamekuwa wakisafirisha Madini yao kwenda kuuza umbali mrefu ambapo viwanda vinapatikana huku miundombinu ya usafirishaji malighafi hizo ikiwa na changamopo hivyo, viwanda hivyo vitakuwa suluhisho la changamoto za usafirishaji na masoko kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini hayo.

Pia, Waziri Mavunde amesema kwamba ujenzi wa viwanda kuongeza thamani madini ya shaba na nikeli unaendelea maeneo mengi nchini ikiwemo Lindi na Chunya,Mbeya na kutoa rai kwa mikoa kutenga maeneo maalum ya ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani Madini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter