Wananchi wa Kisiwa cha Maisome kilichopo katika ziwa Victoria wilayani Sengerema watamegewa hekta 2943.8 kutoka katika Hifadhi ya Msitu wa Maisome kwa ajili ya Malisho ya Mifugo.
Naibu waziri wa Maliasili na Utalii Dunstan Kitandula amesema hayo Bungeni Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Buchosa Eric James Shigongo aliyetaka kujua ni lini Serikali itawamegea eneo wananchi wa Visiwa vya Maisome katika Hifadhi ya Kisiwa cha Maisome.
Kitandula ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua katika kutekeleza maelekezo ya Baraza la Mawaziri kwa kufanya mapitio ya mpaka wa msitu wa hifadhi ya Maisome ambapo hekta 2943.8 zitatolewa kwa wananchi na eneo hilo kubakiwa na hekta 9319.2.
”Kwa sasa taratibu za kubadili mpaka kisheria na kupata ramani mpya zinaendelea. Mara zoezi hilo litakapokamilika Mheshimiwa Mbunge pamoja na Wananchi watajulishwa ambapo watakuwa na muda wa siku 90 kutoa maoni yao kabla ya tangazo rasmi la kutangaza eneo jipya la hifadhi baada ya mabadiliko niliyoyasema hapo juu” ameongeza Kitandula.
Katika hatua nyingine Kitandula amesema kuwa katika kutatua changamoto za mwingiliano wa shughuli za uhifadhi na zile za kibinadamu, Serikali iliwasilisha taarifa ya umuhimu wa kumega hifadhi hiyo kama sehemu ya utatuzi wa migogoro ya vijiji 975.