Kufuatia ongezeko la kodi la maziwa yanayotoka nje ya nchi, wafugaji wa ng’ombe kutoka Nyanda za Juu Kusini wamesisitizwa kuchangamkia fursa hiyo ya soko kwa kuongeza juhudi ya kuzalisha maziwa ili kukidhi mahitaji ya wateja na watumiaji wa bidhaa hiyo nchini na wao kupata faida zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Ali Hapi, amesema hayo wakati wa mkutano maalum wa kuwajengea uwezo wafugaji pamoja na wadau wa sekta ya maziwa kutoka Iringa na Njombe na kueleza kuwa, mkoa huo umetenga maeneo maalum kwa ajili ya wawekezaji waliojikita katika shughuli za mifugo ambapo hekta 1,024,000 kwa ajili ya ufugaji. Katika ya hizo, hekta 20,000 zipo Kilolo, Iringa vijijini hekta 98,000, Manispaa hekta 6,500 na Mufindi hekta 157.
“Watanzania hawajachangamkia fursa hii ya kufuga kisasa kwa sababu kiwanda cha Asas pekee kinahitaji maziwa lita 50,000 kwa siku lakini kinapata lita 25,000 kwa siku. Tunataka mfuge kisasa, ng’ombe wachache lakini wenye faida, unawaangalia vizuri kwa kuzingatia ushauri wa wataalamu ili watoe maziwa mengi na kuondokana na kufuga”. Amesema Hapi.