Na Mwandishi wetu
Ukosefu wa wodi ya wazazi, nishati ya umeme na vifaa tiba vya kutosha umepelekea wakinamama wajawazito kujifungulia sakafuni, licha ya kituo cha afya kupandishwa hadhi baada ya malalamiko ya wananchi kutumia muda mrefu mpaka kufikia huduma za afya.
Kituo cha afya cha Ikoho kilichopo Kata ya Maendeleo wilayani Mbeya kinakumbwa na changamoto kubwa katika utoaji huduma kwa wajawazito. Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa kituo hicho, Japhary Leonard, kituo cha Ikoho hupokea wajawazito takribani 20 na ni chumba kimoja tu ndicho hutoa huduma za kujifungulia.
Harambee iliyofanyika hivi karibuni imefanikiwa kukusanya Sh milioni 5, huku ni jumla ya Sh milioni 73 ikihitajika kukamilisha jengo hilo ambalo awali wakazi zaidi ya 800 walijitolea kujenga. Katika harakati za upatikanaji wa fedha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mbeya, Mwalingo Kisemba ametaka kila mwananchi katika kata hiyo kukusanya Sh 20,000 hadi kufikia Oktoba wakati harambee nyingine itakapofanyika.
Akizungumza na wananchi katika kata hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Amerchiory Kulwizira ambaye alijitolea mifuko 20 ya saruji ili kuunga mkono ujenzi huo amewashukuru wananchi kwa juhudi zao na kuahidi kuwa serikali itamalizia ujenzi huo pamoja na miundombinu yote inayohitajikana pia kuweka vifaa tiba.