Kwa hali ya kawaida mawazo ya kuacha kazi huwajia wafanyakazi wengi, kutokana na mambo wanayopitia katika kazi zao. Lakini hali hiyo mara nyingi huwa ya muda mfupi, na mwisho wa siku, jambo la msingi ni kuangalia namna ambayo unaweza kutimiza malengo yako. Ni kweli kuwa kuna changamoto mbalimbali katika ajira lakini uamuzi wa kuacha kazi ni mkubwa na hautakiwi kuchukuliwa kirahisi. Ni muhimu kuwa na mpango kama unafikiria kuacha kazi uliyonayo.
Hivyo ikiwa una mpango wa kuacha kazi, ni vyema kuzingatia haya kabla ya kufanya maamuzi:
Akiba
Kila mfanyakazi anatakiwa kujiwekea mazoea ya kuweka akiba, ili kuweza kukabiliana na majukumu ya maisha. Akiba inaweza kumsaidia mfanyakazi pindi anapoacha kazi hivyo hakikisha kuwa una akiba ambayo itakusaidia kipindi huna njia ya kuingiza kipato. Ikiwa huna akiba basi tambua kuwa maamuzi yako ya kuacha kazi yanaweza kuathiri mwenendo wako wa maisha kwa sababu utahitaji fedha kwa ajili ya matumizi ya kila siku.
Utafanya nini baada ya kuacha kazi?
Ni muhimu kupanga mipango sawa sawa kabla ya kuacha kazi, hivyo hakikisha unajua nini utafanya baada ya hapo. Kwa mfano kama unataka kujiajiri, hakikisha kuwa mipango yote ipo sawa na baada ya kuacha kazi unaenda moja kwa moja kusimamia biashara au kampuni yako.
Muda
Siku zote. kitu kinachofanyika katika muda sahihi huleta matokeo chanya. Zingatia muda na tafakari, je ni muda sahihi kuacha kazi yako na kufanya mambo mengine? Kuacha kwako kazi hakutakiwi kuharibu mikakati, na mfumo wako wa maisha na badala yake, kunatakiwa kuleta maendeleo na mabadiliko mazuri zaidi.
Stahiki
Unapoajiriwa unaingia makubaliano na muajiri, hivyo hakikisha kuwa unapoacha kazi muajiri wako atakupa haki zako kwa mujibu wa Sheria na makubaliano yenu. Ni muhimu kujua sheria na masharti ya kuacha kazi katika kampuni ili kuepusha usumbufu wowote unaoweza kutokea baadae.
Kwa ufupi, kuacha kazi ni suala zito na kila mtu anatakiwa kufikiria kwa makini na kuangalia kama mazingira yanaruhusu kabla ya kufanya maamuzi yoyote. Pia unaweza kuomba ushauri kutoka kwa watu mbalimbali ili kupata picha halisi ambayo itakusaidia kufanya uamuzi sahihi.