Home VIWANDANISHATI Songas yalipa gawio la TZS 8.8 bilioni kwa Taasisi za Serikali

Songas yalipa gawio la TZS 8.8 bilioni kwa Taasisi za Serikali

0 comment 120 views

Songas Limited, kampuni ya kitanzania inayoongoza kwa kuzalisha umeme kwa kutumia nishati ya gesi, imeilipa serikali TZS 8.8 bilioni, kama gawio la hisa zake katika kampuni.

Kampuni ya Songas Limited ni mshirika wa serikali katika kufikia mahitaji ya nishati ya umeme nchini Tanzania na umiliki wake unajumuisha taasisi za nishati – Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Tanzania Development Finance Company Limited (TDFL) pamoja na Globeleq, kampuni binafsi ya uzalishaji wa umeme yenye shughuli zake barani Afrika.

Afisa Mkuu wa Fedha wa Songas Limited, Bw. Anael Samuel, amesema TANESCO itapokea TZS 2.2 bilioni huku TPDC ikipokea TZS 6.6 bilioni, kila gawio litakatwa kodi ya zuio (withholding tax) na pia kiasi hicho kimetokana na uwiano wa hisa zinazomilikiwa na taasisi hizo kwenye kampuni ya Songas.

Serikali pia inanufaika kupitia 32% ya hisa zake katika TDFL, inayopokea TZS 1.8 bilioni kama gawio.  Vile vile, serikali itanufaika kupitia kodi ya zuio kwenye gawio inayokusanywa na TRA.

Songas imelipa jumla ya shilingi za kitanzania bilioni 121.6 tangu mwaka 2012 kama gawio kwa serikali na tasisi zake, na pia kuchangia shilingi za kitanzania bilioni 139.3 kama kodi za mapato ya kampuni.

“Tangu mwaka 2004, Songas imekuwa ikiwezesha dhamira ya kuipeleka Tanzania katika uchumi wa viwanda kwa kuchangia takribani 20% ya nishati ya uhakika na kwa bei nafuu katika gridi ya taifa, huku ikiendelea kusambaza gesi asilia katika viwanda mbalimbali, Dar es Salaam.  Songas inatoa mbadala wa nishati kwa gharama nafuu na kuiweka kampuni kama mzalishaji muhimu wa nishati katika ukanda huu” alisema Bw. Nigel Whittaker, Mkurugenzi Mtendaji wa Songas Limted

Bw. Whittaker aliongeza kuwa kampuni inampango wa kuongeza uzalishaji kutoka 180MW mpaka 250 MW ili kufukia mahitaji ya nishati yanayokuwa kwa kasi sana na kuchangia katika sera ya ukuwaji wa viwanda nchini.

Kwa sasa Songas anaongoza kwa kuzalisha nishati kwa bei nafuu katika ukanda wa Afrika Mashariki kwa kutumia nishati ya gesi inayopatikana nchini. TPDC inakadiria tangu kuanza kwa shughuli za Songas 2004, kampuni imeokoa takribani TZS 11 trilioni kwa uchumi wa Tanzania.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter