Home BIASHARA Sababu 5 za kutumia video kujitangaza

Sababu 5 za kutumia video kujitangaza

0 comment 112 views

Imekuwa ni kawaida kuona bidhaa na huduma zinatangazwa katika mfumo wa picha. Je wajua kuwa mfumo wa video pia una manufaa makubwa katika utangazaji wa bidhaa au huduma? Inaelezwa kuwa 63% ya wafanyabiashara wameanza kutumia video kutangaza biashara zao na wengi wao wameeleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kutumia mfumo huo.

Kama ilivyo katika picha, mfanyabiashara anaweza kurekodi video kuhusu bidhaa au huduma zinazopatikana katika biashara yake aidha kwa kutumia wataalamu wa video au anaweza kurekodi yeye mwenyewe kwa kutumia simu ya mkononi, jambo la msingi ni kuwa mbunifu ili kuwavutia wateja wengi. Pia video hizo anaweza kuzitangaza katika mitandao kwa sababu watu wengi siku hizi hutumia muda mwingi katika mitandao ya kijamii na intaneti.

Hizi hapa ni sababu zinazoelezea umuhimu wa kutangaza bidhaa au huduma kwa kutumia mfumo wa video.

Mauzo ya moja kwa moja: Utafiti unaonyesha kuwa asilimia 74 ya watu ambao hutazama video huhamasika kununua bidhaa hiyo moja kwa moja. Ni kawaida kushawishika zaidi baada ya kuona kitu, hivyo kama picha huhamasisha watu kununua bidhaa, basi ni dhahiri kuwa video itahamasisha wateja wengi zaidi ili mradi tu ziandaliwe katika ubunifu wa hali ya juu.

Hujenga uaminifu: Uaminifu ni moja ya mambo ya msingi katika biashara. Nia ya kutangaza bidhaa au huduma ni kujenga mahusiano ya muda mrefu na uaminifu wa kudumu baina yako (mfanyabiashara) na wateja. Kwa kutengeneza machapisho ya aina mbalimbali, wateja watakufuata kila wanapokuwa wanahitaji bidhaa au huduma. Kutokana na wateja wengi kuendelea kuwa na wasiwasi kuhusu biashara mitandaoni, hali mbayo inasababishwa na baadhi ya wafanyabiashara kuwa wadanganyifu, video huonyesha uhalisia zaidi kuliko picha hivyo ni rahisi kwa mteja kuamini kile anachokiona.

Ni rahisi kuelezea kila kitu: Unataka kuzindua bidhaa au huduma mpya? Tengeneza video kuonyesha jinsi bidhaa au huduma hiyo inavyofanya kazi. 98% ya wateja wanasema wametazama video ya ufafanuzi ili kujifunza zaidi juu ya bidhaa au huduma. Pia inaelezwa kuwa watu wengi huvutiwa na video zinazotengenezwa kwa michoro hivyo ikiwa unataka kuelezea biashara unaweza kutengeneza video katika mfumo wa michoro ili kuleta maana zaidi.

Husaidia wasiopenda maelezo marefu: Wateja wametofautiana na kuna wale ambao hawaoni shida kusoma tangazo lenye maelezo mengi na wakati huo huo, kuna wale ambao wakiona tangazo lina maelezo marefu basi wanaachana nalo. Wateja wengi wa kisasa hufurahia matangazo yenye maelezo mafupi na njia nzuri kwa mfanyabiashara ni kupitia video. Ni muhimu kuwafirikia wateja wote na kutumia njia mbalimbali za matangazo ili kuwafikia.

Ni rahisi kutumiana video: Hii ipo zaidi katika mitandao ya kijamii ambapo watu wengi hupenda kutumiana video. Takribani 76% ya watu hutuma video zinazowaburudisha kwa marafiki zao. Jenga tabia ya kutengeneza video zinazofurahisha na kuhamasisha ili watu wanapoziona wazitume kwa watu wengine. Hii itasaidia biashara yako kujulikana zaidi.

Kutokana na maboresho ya teknolojia, matangazo ya video yanazidi kuwa nafuu na ni rahisi kwa matangazo hayo kuenea kwa haraka katika maeneo mbalimbali duniani. Ni muhimu kwa wafanyabiashara kuwa wabunifu, kwenda sawa na mabadiliko na kufikiria kama mteja ili kutengeneza matangazo yenye maana na yanayohamasisha wateja.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter