Kutokana na maboresho ya teknolojia, matumizi ya nywila/nenosiri yamekuwa ni kawaida kwa wengi wetu katika kuhifadhi taarifa zetu muhimu au kuweza kuzifikia taarifa muhimu katika mtandao au vifaa vya kielektroniki. Siku zote inashauriwa kutengeneza nywila isiyo rahisi ili kuepuka upotevu wa nyaraka muhimu au kutapeliwa. Katika upande wa biashara, jambo hilo ni muhimu ili kuepuka kutapeliwa na wateja kupitia mtandao au kupoteza nyaraka muhimu za biashara.
Ni mambo gani ya kuepuka kwa ujumla?
Epuka kutumia namba pekee
Hakuna mtu ambaye hufurahia kusahau nywila yake. Lakini hiyo isiwe sababu ya kutumia namba peke yake kutengeneza nywila. Na wengi hupenda kutumia namba rahisi kama 12345678 au 1111 jambo ambalo si salama kwani ikiwa mtu anataka kufikia kwa mfano taarifa za kifedha katika akaunti ya biashara itakuwa ni jambo rahisi sana kufanya hivyo kupelekea taarifa za biashara kuwa katika hali hatarishi. Pia epuka kutumia tarehe za kuzaliwa kwani nazo ni rahisi mtu kuhisi. Ikiwa unajali usalama wa taarifa za biashara yako kwa ujumla hakikisha unatengeneza nywila yenye nguvu na salama zaidi kila sehemu.
Epuka kutumia majina ya utani/ndugu
Sio salama kutumia majina ya utani au ya ndugu kutengeneza nywila yenye nguvu, kwani hiyo imepelekea watu wengi kutapeliwa na kupoteza taarifa muhimu kwa sababu ya matumizi ya majina ya utani au watu wa karibu kwa kuwa ni rahisi kwa watu wengine kuyafahamu.
Usitumie programu za kutengenezea nywila
Programu za kutengenezea nywila (password generators) si salama katika utengenezaji wa nywila imara kwa sababu ni rahisi kwa matapeli (hackers) kutambua nywila zilizotengenezwa katika programu hizo. Kama unataka kutengeneza nywira imara hii si njia sahihi ikiwa unataka kuepuka utapeli au upotevu wa taarifa binafsi au za biashara.
Usiandike mahali
Wengi hupenda kuandika taarifa muhimu ili wasisahau jambo ambalo si sahihi na linaweza kuleta athari ikiwa mtu mwenye nia mbaya ataona nywila yako. Kwa sababu za usalama zaidi ni vyema kujitahidi kuikumbuka nywila kichwani kuliko kuandika mahali.
Usitumie nywila moja kila mahali
Watu wengi huona kuwa ni rahisi kutumia nywila moja kila sehemu. Hii inaweza kuhatarisha maeneo mengi kwa wakati mmoja kwa mfano mtu anaweza kuwa anatumia nywila moja katka barua pepe, katika akaunti ya benki, mitandao ya kijamii nk. Ikitokea tapeli amejua nywila husika ni dhahiri kuwa maeneo mengi yanaweza kuathiriwa kwa wakati mmoja.
Usimpe mtu mwingine nywila yako
Kumekuwa na kawaida ya kupeana nywila kutokana na kuaminiana lakini hali hiyo inaweza kuleta changamoto ikiwa mtu uliyempa nywila yako akatumia kwa nia mbaya. Ili changamoto zozote, nywila yako inatakiwa kuwa siri yako peke yako.
Pamoja na hayo, ni muhimu kwa watu kuacha kupuuzia suala la uimara wa nywila katika maeneo yote yanayohitaji myumiaji kuna nayo, pia ni muhimu kujitahidi kubadilisha nywila kila baada ya muda ili kuhakikisha taarifa na nyaraka zote zipo salama kila wakati.