Mbali na kilimo kuwa ni tegemeo la watanzania wengi (takribani 70%) katika kujipatia kipato na kujikimu kimaisha, watu wengi wanaendelea kunufaika zaidi kupitia kilimo hususani kilimo cha mbogamboga. Siku zote huwa inashauriwa kufanya mambo ambayo tunafurahia kuyafanya ili kuweza kuyafanya mambo hayo kwa ustadi zaidi na juhudi ya hali ya juu ili kuweza kupata mafanikio zaidi, huo unaweza kuwa ushauri mzuri lakini muda mwingine watu huwa hawajui ni mambo gani wanafurahia kuyafanya hadi wajaribu mambo hayo kwa mara ya kwanza.
Katika Sekta ya Kilimo, ni dhahiri kuwa watu wengi hasa vijana hawaifurahii sekta hii licha ya kuwepo na ushuhuda kutoka kwa vijana mbalimbali waliofanikiwa kupitia kilimo. Ingawa serikali imekuwa ikiendelea kutoa hamasa kuhusu kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na kutoa nyenzo za kisasa, mafunzo zaidi yanahitajika ili kuweza kuchanganua sekta hii kwa undani zaidi ili vijana waweze kuona ni fursa gani wanaweza kuzitumia katika sekta hii ili kuweza kujipatia kipato na kupata mafanikio ya kiuchumi- binafsi na ya taifa kwa ujumla.
Kilimo cha mboga si lazima kifanyike katika eneo kubwa, ndio maana siku hizi kuna mifumo mbalimbali ambayo haihitaji nafasi kubwa kufanya kilimo hikikwamfano mfumo wa vitaru wa (Greenhouse) ambao hufanywa na wakulima hasa sehemu za mjini kutokana na kutokuwepo na maeneo makubwa ya kufanya kilimo. Hivyo kulingana na ukubwa wa eneo lako unaweza kufanya kilimo cha bustani ya mboga (ndani-greenhouse au nje-kwenye ardhi kama ilivyo kawaida) na kupata mafanikio. Pia inashauriwa kuanza kuwekeza mtaji kiasi ili kuweza kuona matokeo na kujua mambo gani yaboreshwe na mambo yapi yasiendelelee kufanyika hii kuepusha hasara kubwa ikiwa mambo hayatokwenda sawa.
Hivyo, ili kuweza kufanya kilimo cha mbogamboga na kupata mafanikio kupitia kilimo hicho, yafuatayo ni mambo ya msingi ambayo kila mkulima anatakiwa kujua na kuyazingatia :
Aina mbalimbali za mboga
Hapa mkulima anaweza kuamua ni aina gani ya mboga anataka kujikita nayo baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu aina husika. hivyo zifauatazo ni aina mbalimbali za mboga ambazo mkulima anaweza kulima; aina hizo ni kama nyanya, bamia, bilinganya, matango, pilipili, koliflawa, brokoli, maharage, mchicha, mlenda, chinese, letusi,karoti, vitunguu maji na saumu, spinach na nyingine nyingi.
Eneo
Jua ni muhimu katika kila mimea. Hivyo mkulima anatakiwa kuhakikisha kuwa katika bustani yake ya mboga kuna uwepo wa jua la kutosha ili kurahisisha kuepusha ukuaji wa mimea dhaifu. Pia inashauriwa kuanzisha bustani katika eneo lisilo kuwa na muinuko mkali ili kuepukana na changanmoto ya mmomonyoko wa udongo. Suala moja wapo la msingi kuhusu eneo la bustani ya mboga ni ukaribu wa chanzo cha maji cha kudumu (siku zote maji yanayotumika kumwagilia bustani ya mboga yanashauriwa kutokuwa na chumvi nyingi). Aidha ni muhimu udongo wa eneo husika kuwa na rutuba, na kupitisha maji kwa urahisi. Vile vile inashauriwa kupanda miti pembezoni mwa bustani ya mboga ili kuepukana na athari zinazoweza kutokea kutokana na upepo mkali, na maambukizi ya magonjwa yanayoweza kutokea kutokana na upepo.
Upandaji
Hapa hutegemea na mfumo ambao mkulima atatumia. Ikiwa mkulima atachagua kutumia teknolojia za kisasa kama Greenhouse za kawaida, au Greenhouse za Hydroponics basi hapa suala la fedha litahitajika ili kuweza kununua mfumo husika na kuutayarisha kwaajili ya upandaji wa mboga. Ikiwa mbogamboga husika zitapandwa katika ardhi ya kawaida basi ni muhimu kwa mkulima kuhakikisha kuwa udongo unatifuliwa vizuri, na kuinua matuta kidogo ili kuzuia maji yasituame. Pia ni muhimu kumwagilia siku moja kabla ya kufanya upandaji ili udongo uwe na unyevu wa kutosha. Umwagiliaji usipite kiasi kwani mizizi inaweza isiote. Aidha kikawaida mbegu ndogo hupandwa katika kina kifupi ikiringanishwa na mbegu kubwa ambazo hupandwa katika kina kirefu zaidi. Siku zote mkulima anashauriwa kupanda mbegu bora,zilizokauka,na kukomaa, ambazo hazijashambuliwa na wadudu ili kuweza kupata matokeo mazuri.
Mbolea na Dawa
Ili kuweza kupata mimea yenye afya na bora kuna umuhimu wa kutumia mbolea na dawa. Hivyo kutokana na mfumo wa bustani husika virutubisho huongezwa katika mimea ili kuweza kuhakikisha mimea inakua vizuri. Kwamfano katika mfumo wa hydroponics kuna mfumo maalum ambao hutumika kuweza kuipa mimea virutubisho vyote vinavyohitajika, huku katika bustani za kawaida mkulima anaweza kuweka samadi ya kawaida kwa mikono ili kuongeza virutubisho katika mimea na dawa kama Calcium Almonium Nitrate (CAN), Urea, NPK na nyinginezo zinaweza kuwekwa kwa vifaa kama pump. Hivyo ni muhimu kwa mkulima kutumia njia stahiki ili kuweza kupata matokeo yanayoridhisha zaidi.
Soko
Katika kila uwekezaji soko huwa ni muhimu sana kwani bila soko hakuwezi kuwa na faida. Hivyo wakati wa utafiti wa aina ya mboga unayotaka kujikita nayo inashauriwa kufanya utafiti wa soko pia ili kuweza kujua ni wateja wa aina gani utakuwa ukiwauzia mboga unazotaka kulima ili mboga hizo zikishakuwa tayari ziweze kuwafikia wateja husika wakati bado zina hali nzuri, kwani wateja wengi huvutiwa na mimea ambayo imetoka moja kwa moja shambani na bado iko katika hali nzuri. Unaweza kujikita na soko la ndani au la nje na kuweza kupata mafanikio, utafiti na kuunda mtandao kunaweza kurahisisha suala zima la utafutaji wa masoko. Kwamfano Mjasiriamali na mkulima Hadija Jabiry, ni mmoja wa wakulima mashuhuri nchini ambaye amejikita katika uuzaji wa mbogamboga katika soko la nje kupitia brandi yake ya ‘Eatfresh’ iliyopo chini ya GBRI Business Solutions Limited baada ya kufanya utafiti wa kutosha na kugundua kuwa mbogamboga anazozalisha zina soko kubwa katika nchi za Ulaya.
Mbali na hayo, ni muhimu kuwa mvumilivu, jasiri na mtu ambaye yuko tayari kwenda sawa na mabadiliko yanayotokea duniani. Kwani si kila wakati mambo huenda kama inavyokuwa imepangwa, hivyo ni muhimu kupata mafunzo kila inapowezekana, kujua maboresho mapya ya teknolojia katika upande wa kilimo na kuchukua hatua stahiki ili kuweza kurahisisha ufanisi wa kazi na kupata mavuno zaidi ili kuweza kutosheleza mahitaji ya soko.