Na Mwandishi wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Balozi wa Cuba nchini, Lucas Podello na kuwakaribisha wafanyabiashara wa Cuba kuja kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya dawa. Majaliwa amesema serikali ya Tanzania kwa sasa inaagiza dawa kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa hivyo kuwepo kwa kiwanda cha dawa nchini kutapunguza gharama kwa kiasi kikubwa.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa yupo nchini Cuba kwa ziara ya kikazi inayolenga kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili amesema serikali imejipanga kuendeleza sekta ya viwanda nchini kama mkakati wa kukuza uchumi hivyo amewakaribisha wawekezaji kuja kuwekeza nchini hususani katika viwanda vya dawa na sukari.
Majaliwa ameongeza kuwa Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu pia kuna mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo watakaokuja kuwekeza watapata tija. Pia ametumia nafasi hiyo kushukuru serikali ya Cuba kwa kutoa ushirikiano katika masuala mbalimbali ya kiuchumi, kielimu na kijamii nchini humu.
Balozi Podello naye amesema nchi ya Cuba itendelea kutoa ushirikiano kwa Tanzania huku akipongeza jitihada zinazofanywa na serikali katika kuboresha maendeleo na kukuza uchumi.