Home LifestyleHealth & Fitness MADAKTARI TANZANIA WAOMBA KUKINGWA NA VIRUSI VYA CORONA

MADAKTARI TANZANIA WAOMBA KUKINGWA NA VIRUSI VYA CORONA

0 comment 163 views

Chama cha madaktari Tanzania MAT, kimeitaka serikali kuhakikisha inaongeza vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya katika kipindi ambacho watakuwa wanahudumia wagonjwa na wakisiwa wa maambukizi ya virusi vya corona.

Idadi ya visa vya maambukizi ya virusi vya Corona nchini Tanzania imethibitishwa kufikia ishirini, kukiwa na kifo kimoja huku waliopona ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi hivyo wakiwa ni wawili.

Katika hali kama hii chama cha madaktari kinatoa tahadhari ya mapema kwa mamlaka yenye dhamana ya kushughulikia masuala ya afya kuhakikisha wanakuwa na idadi ya kutosha ya vifaa vya kujikinga kwa wahudumu wa afya ambao nao wamekuwa ni wahanga wakubwa ulimwenguni kwani baadhi yao wamepata maambukizi wakiwa wanatoa huduma kwa wagonjwa.

Rais wa chama hicho daktari Elisha Osat amewaambia wanahabari kuwa, ili watumishi wa afya waweze kufanya kazi katika Mazingira salama wanahitaji kulindwa, hivyo vifaa kama vile barakoa na mavazi ya kufunika mwili mzima hayatakiwi kukosekana katika maeneo ambayo yametengwa kuwahudumia wagonjwa na wote wanaokisiwa kuwa wameambukizwa virusi vya Covid-19

Wakati chama hicho cha madaktari kiikitoa ombi hilo, changamoto ya mavazi ya kujikinga kwa wahudumu wa afaya wakati wakitoa huduma imezikumba nchi kadhaa ulimwenguni, ikitajwa kutokana na kuzorota kwa uzalishaji wa viwandani, na kuvurugika kwa huduma za usafirishaji ulimwenguni kutokana na nchi nyingi kufunga mipaka yake katika juhudi za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Katika hatua ya chama hicho cha madaktari kuhakikisha hakuna mrundikano wa wagonjwa wanaokwenda kliniki kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali, wameiomba serikali kuhakikisha walau wagonjwa wa maradhi sugu ikiwemo shinikizo la damu na kisukari wanapatiwa dawa za muda mrefu, hatua ambayo haita wahitaji kufika hospitalini mara kwa mara na kusababisha mrundikano ambao huenda ukachochea kuongeza kasi ya maambukizi ya virusi hivyo. Shadrack Mwaibambe, Rais Mteule wa MAT anasema.

Msisitizo wa viwanda vya ndani kufanya uzalishaji wa bidhaa kama vile dawa na mavazi ya kujikinga umekuwa ukitolewa mara kadhaa na wadau wa maendeleo ya viwanda ili kuhakikisha nchi haikumbwi na uhaba hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliana na maradhi ya Corona.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter