Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIBIASHARA Vidokezo muhimu vya usimamizi wa muda

Vidokezo muhimu vya usimamizi wa muda

0 comment 122 views

Ni kawaida kuona mtu ameajiriwa huku amejiajiri ili kuongeza kipato chake. Kuajiriwa na kujiajiri si jambo dogo na mtu anatakiwa kujipanga ili kuweza kufanya mambo haya mawili kwa pamoja, la sivyo anaweza kujikuta anapoteza vyote kwa sababu ya kutokuwa makini. Kawaida ni rahisi kwenda na wakati/muda ukiwa kazini, hivyo unatakiwa kupangilia muda wako hata katika shughuli yako ambayo unaifanya kwa muda.

Fanya hivi kupangilia muda wako katika ujasiriamali wako ili mambo yaweze kwenda sawa, katika pande zote:

Jenga kawaida ya kutengeneza orodha ya mambo ya kufanya. Orodha hiyo jitahidi kutengeneza usiku ili asubuhi ukiamka uendelee na mambo yako kulingana na orodha hiyo. Hakikisha mambo uliyoyaweka katika orodha yako utamudu kuyafanya kwa siku hiyo, hivyo usiweke mambo mengi sana au mambo ambayo yako nje ya uwezo wako.

Achana na mambo yasiyokuwa na umuhimu/vikwazo ukiwa unafanya kazi yako ya pili. Baadhi ya mambo ambayo unaweza kuachana nayo ni pamoja na kuangalia televisheni, kushinda katika mitandao ya kijamii, mazungumzo yasiyo na umuhimu na marafiki. Hii itakusaidia kufanya mambo yako ndani ya muda na kuendelea na shughuli nyingine.

Kuna baadhi ya watu ambao ikifika asubuhi tu wanakuwa na nguvu, akili yao inakuwa makini kushughulika na kazi zote muhimu na watu wengine jioni ndio muda wao wa kufanya mambo kwa umakini zaidi. Hivyo tafakari ni muda upi unakuwa na utayari, na umakini wa kufanya mambo ya muhimu ili kuhakikisha kila ikifika muda huo mambo yote ya muhimu yanafanyika, hii itabadilisha sana shughuli yako.

Jambo lingine la muhimu ni kuacha kufanya kazi nyingi kwa muda mmoja, pangilia mambo yako vizuri. fanya kazi moja ukimaliza endelea na kazi nyingine. Kuchanganya kazi nyingi kwa muda mmoja kunaweza kupelekea matokeo kutokuwa mazuri na lengo la kuanzisha shughuli nyingine mbali na kazi yako ni kupata maendeleo zaidi na si changamoto ambazo haziishi.

Sawa una uwezo wa kufanya kila kitu mwenyewe. Lakini unashauriwa kuwapa watu wengine hasa wataalamu wa jambo husika kukusaidia katika shughuli yako ili matokeo yazidi kuwa mazuri zaidi. Hivyo kama unaweza kuajiri mtu mwingine basi fanya hivyo lakini hakikisha maamuzi hayo hayaingiliani na masuala ya fedha kwa namna moja au nyingine.

Vilevile, sio lazima kukubali kila kazi utakayoletewa, muda mwingine utakuta mteja amekuja na unamjua kabisa tabia yake aidha ya kuchelewesha malipo, lugha mbaya nk si lazima ukubali kufanya naye kazi, mara nyingine kusema hapana ni njia moja wapo ya kutunza muda wako na kufanya mambo mengine yenye umuhimu zaidi na fedha zaidi. Hivyo ikiwa inakubidi kusema hapana basi fanya hivyo ili kuendelea na mambo mengine ya muhimu katika shughuli yako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter