Home BENKI Umemfungulia mwanao akaunti ya benki?

Umemfungulia mwanao akaunti ya benki?

0 comment 32 views

Miaka ya hivi karibuni tumeshuhudia watanzania wengi zaidi wakijiunga na huduma za kibenki kutokana na jitihada mbalimbali ambazo taasisi za fedha zimekuwa zikifanya katika kuhakikisha wananchi wanaelimika na kuhamasika kuanza kutumia mifumo rasmi ya utunzanji wa fedha huku wakiachana na ile waliyoizoea.

Japokuwa suala hili limeonyesha mafanikio kwa kiasi kikubwa, bado kuna changamoto ambazo sio rahisi kuzifumbia macho. Japokuwa idadi kubwa ya wananchi wamebadili mtazamo na kuanza kutumia mifumo rasmi kutunza fedha zao, watoto wameonekana kusahaulika katika mabadiliko haya.

Asilimia kubwa ya wazazi, walezi au hata wananchi wa kawaida wanadhani kuwa labda huduma za kibenki zipo kwa ajili ya watu wazima tu, yaani wale wote waliotimiza miaka 18 na kuendelea ambao kisheria wanatambulika kama watu wazima. Ingawa taasisi mbalimbali za fedha zimekuwa na programu maalum kwa ajili ya watoto chini ya umri wao, wengi wanaonekana kutokuwa na taarifa au maarifa kuhusu huduma hii muhimu ambayo imeanzishwa hususani kwa ajili ya watoto.

Kwa upande wao, Benki ya NMB inayo akaunti maalum inayofahamika kama NMB Mtoto Akaunti ambapo walengwa wakuu ni watoto japokuwa kisheria inaendeshwa na ipo chini ya wazazi au walezi. Akaunti hii inalenga kutunza akiba ya mtoto na kiwango chake rafiki cha riba kinawezesha akiba kuendelea kukua. Mbali na masuala ya riba, NMB Mtoto Akaunti inafunguliwa kwa kiasi kidogo cha Sh. 10,000 tu za kitanzania hivyo gharama hii ndogo inaruhusu wazazi/walezi kutoka hata familia zile za chini kumudu gharama na kuwekeza kile kidogo walichonacho kwa ajili ya watoto wao.

Kama mzazi/mlezi unaweza ukawa unajiuliza ni kwanini hasa ufungue akaunti kwa ajili ya mtoto/watoto wako? Kwanini usiwatunzie akiba katika akaunti yako binafsi? Ni kwa sababu gani ufanye hivyo japokuwa hawatoweza kutumia fedha hizo kwa wakati huo? Maswali haya ni baadhi tu katika yale mengi ambayo labda wazazi hujiuliza wanapoambiwa kuwa hata watoto nao wanaweza kufunguliwa akaunti za benki.

Ukweli ni kwamba kuna faida nyingi tu za kufanya hivyo. Kwa taasisi ya NMB, programu yao ya watoto akaunti mbali na kutoa riba ambayo humpa mteja zaidi, pia inasaidia kumjengea mtoto nidhamu ya kutunza fedha na kuwa na akiba ambayo itamsaidia katika maisha ya baadae. Akiba ya mtoto pia inampatia uhakika wa masuala muhimu kama elimu, afya na ustahimilivu wa maisha. Kuweka akiba pia kunamsaidia mtoto kupanga matumizi yake mwenyewe pindi anapofikia umri wa kumiliki fedha zake kihalali.

Kama wanavyofanya NMB, benki nyingine zinapaswa kuwa na akaunti maalum kwa ajili ya wazazi kuweka akiba ya watoto wao na isiishie hapo tu, wanapaswa kuingia mitaani na kuwaelimisha wananchi hususani wale wenye maisha ya kati na ya chini kuhusu umuhimu wa kuwa na akiba ya watoto kwani kufanya hivyo ni mojawapo ya kuwahakikishia kuwa watapata mahitaji yao ya msingi huko baadae.

Vilevile, jukumu hili lisibaki kwa taasisi za fedha pekee. Wazazi na walezi wanapaswa kujenga mazoea ya kuzungumza na watoto wao kuhusu hali yao ya kifedha. Katika ulimwengu huu wa utandawazi ni muhimu sana kwa wazazi kuwa huru kuzungumza masuala ya kifedha na watoto wao. Kwa kufanya hivyo, watoto nao wanapata ufahamu kuhusu namna ambazo wanaweza kusaidia kutunza fedha, kujiwekea akiba na hata kuwasaidia wazazi wao pale wanapoweza. Jamii kwa ujumla inapaswa kubadilika hasa katika mambo yanayohusu fedha na wazazi kujitokeza kwa wingi kufungua akaunti kwa ajili ya watoto wao ni hatua kubwa kuelekea ulimwengu mpya kabisa wa huduma za kibenki na faida zake lukuki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter