Home BIASHARA Unafahamu kilimo cha Hydroponics?

Unafahamu kilimo cha Hydroponics?

0 comment 137 views

Hydroponics ni nini? Hii ni njia ya kulima bila kutumia udongo, mimea hukua kwenye mabomba au chaneli maalumu ambazo hupitishiwa virutubisho ambavyo huwa vinakuwa kwenye maji na kwenda katika mzizi wa mimea.

NASA wamewahi kusema  kuwa kilimo cha hydroponics ni kilimo cha siku zijazo ambacho kitatumika kukuza vyakula nje ya dunia. Wakulima wengi wanaofanya kilimo hiki hukuza zaidi mboga na matunda huku wakitumia teknolojia ya green house.

Faida zake:

Kuna baadhi ya maeneo hakuna ardhi ya kutosha au ardhi haifai kulima mimea. Hivyo kwa kupitia mfumo wa hydroponics, wakulima wanaweza kuendelea kulima na kujipatia mazao na hivyo kuepusha njaa katika maeneo husika.

Kilimo hiki hakichukui nafasi kubwa hivyo unaweza kufanya kilimo hiki hata katika maeneo madogo na kujipatia mazao pia.

Inaelezwa kuwa mimea ambayo hukua katika mfumo huu huwa inatumia 10% tu ya maji kuliko mimea inayokua katika ardhi. Hivyo mkulima hatakiwi kuhofia suala la maji sana ikiwa atafanya kilimo hiki. Na mara chache tu mimea inaweza kukosa maji kama mfumo huu umepasuka mahali hivyo mkulima anatakiwa kuwa makini kuepusha hilo.

Hakuna suala la magugu katika mfumo huu hivyo mkulima hawezi kupoteza muda wapi kutoa magugu kama ilivyo katika kilimo kingine. Pia mimea inayokuzwa katika mfumo huu huepukana na magonjwa yanayotokana na udongo.

Hasara zake:

Mkulima asipokuwa makini na kilimo hiki anaweza kupoteza mazao yake. Kwenye ardhi mkulima anaweza kulima na kuacha mimea iendelee kukua, lakini katika mfumo huu mkulima anatakiwa kuichunguza mimea kila siku na kuwa na ujuzi kuhusu mfumo huu ili kuepukana na changamoto yoyote inayoweza kutokea.

Kilimo hiki kinahitaji fedha, kwanza kuunda mfumo huu, pili virutubisho na dawa zinahitaji fedha, umeme unahitajika na maji ya kutosha kuyafikia mabomba hivyo kwa watu wenye kipato cha chini, sio rahisi kulima kwa mfumo huu.

Kuna watu wanasema kilimo hiki si asilia sana kutokana na madawa na virutubisho vinavyowekwa ili kuikuza. Hivyo kwa upande wa soko inaweza kuwa changamoto, hivyo mkulima wa mfumo huu anatakiwa kujua wapi atapata soko. Vilevile ieleweke kuwa si kila kitu ni asilia kwa asilimia mia moja hata katika mimea inayokua kwenye udongo kuna masuala ya madawa pia, na wadudu zaidi kuliko katika kilimo hiki.

Vilevile ni rahisi kwa magonjwa kusambaa katika mfumo huu kwa sababu mimea inazalishwa ndani katika teknolojia ya greenhouse. Wakulima wadogo si muhimu sana kuwaza kuhusu hilo. Lakini kwa wakulima wakubwa wanatakiwa kuwa makini zaidi ikiwa ni pamoja na kutumia maji safi, kucheki mfumo mzima baada ya muda kuhakikisha mambo yanaenda sawa.

Baadhi ya nchi ambazo zimekuwa zikijishughulisha na kilimo hiki tokea miaka kumi iliyopita ni Australia, Tokyo, Netherland na Marekani, inaelezwa kuwa mamilioni ya watu wamepata chakula kutokana na mfumo huu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter