Kutokana na mabadiliko ambayo yamekuwa yakitokea duniani, maboresho katika mambo mbalimbali yamekuwa yakifanyika ili kuweza kuleta urahisi katika maisha ya binadamu. Katika upande wa biashara ‘Incubation’ ni moja ya mambo ambayo yanafanyika kwa sasa ili kuweza kuwasaidia wajasiriamali nchini kuweza kuanzisha biashara zao vizuri, kuzikuza inavyopaswa, kukabiliana na washindani na hata kujenga biashara imara zenye mafanikio makubwa.
Hivyo basi, ‘incubators’ katika biashara ni nini? hizi ni kampuni au mashirika ambayo yamejikita katika kuharakisha ukuaji na mafanikio ya kampuni zinazoanza au ambazo zipo katika hatua ya mwanzo. Kampuni hizo husaidia kampuni zinazoanza katika mfumo wa rasilimali na huduma ikiwa ni pamoja na mitaji, maeneo ya kufanyia kazi, elimu kuhusu namna sahihi ya kufanya biashara, na hata maeneo sahihi ya kujenga mtandao wa kibiashara ili kuweza kufikia malengo ya kampuni hizo.
Inaelezwa kuwa, zaidi ya 50% ya wajasiriamali ni wanawake ambao wengi wao wamekuwa wakifanya ujasiriamali kwaajili ya kupata mahitaji ya kila siku na si katika misingi itakayowapeleka kuteka masoko makubwa duniani. Kutokana na hilo kuna haja kubwa ya kuwahamasisha wajasiriamali nchini hususani wanawake ili kuweza kufanya biashara kisasa, na kuweza kuuza bidhaa zenye viwango vya juu ili kupata faida zaidi baada ya kuteka masoko ya nje.
Kwa Dar es Salaam, wajasiriamali mbalimbali wamenufaika na incubator mbalimbali ambazo zimekuwa zikianzishwa. Wengi wamehamasika kuwasilisha mawazo yao katika incubator hizo kutokana na mitandao ya jamii ambapo incubator hizo zimekuwa zikichapisha taarifa kuhusu mikutano mbalimbali ambayo imekuwa ikifanyika kwa ajili ya kutoa elimu, pamoja na hafla mbalimbali za uvumbuzi katika masuala ya teknolojia pamoja na ujasiriamali kwa ujumla.
Mbali na Shirika la viwanda vidogo nchini (SIDO) kuendelea kutoa elimu,mafunzo na hata kuwasaidia wajasiriamali nchini kuendeleza biashara zao, incubator ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wajasiriamali hasa wanawake, na wadau wa teknolojia ni pamoja na Buni, Ndoto Hub, Teknohama, SafespaceCo, Smart Hub, Impact Hub,Kinu Hub na nyingine nyingi.
Hivyo basi, kupitia incubators hizo, imekuwa ni rahisi kwa wajasiriamali wapya kujua kama biashara wanazotaka kuanzisha au walizoanzisha zitaleta mafanikio mbeleni. Mbali na kuamini wazo la biashara litafanya kazi, kila mjasiriamali mpya anatakiwa kuweka wazo la biashara katika uhalisia ili kuepuka kuanzisha biashara yake wakati ambao si sahihi, kuanzisha biashara au huduma kwa wateja wasio sahihi, na hata kuanzisha bidhaa zinazohitajika kwa msimu( jambo ambalo wajasiriamali wengi wamekuwa wakifanya, hali inayopelekea wengi wao kukosa wateja pindi bidhaa usika ikiwa haihitajiki sokoni).
Kikawaida huwa si rahisi kwa wajasiriamali kupata muongozo kwa watu wenye ujuzi na utaalamu wa tasnia ambazo wanakuwa wamezianzisha. Lakini kupitia incubators, wajasiriamali na wavumbuzi wa masuala mbalimbali hupata fursa ya kupata muongozo kutoka kwa wafanyabiashara ambao wamefanikiwa, wataalamu wenye ujuzi wa tasnia wanazojihusisha nazo ili kupata uzoefu wenye uhalisia. Kwamfano mjasiriamali ambaye anaanzisha mgahawa atapata fursa ya kupata mafunzo na muongozo kutoka kwa wataalamu wanaojihusisha na masuala ya migahawa na hata wajasiriamali ambao wamefanikiwa katika tasnia hiyo.
Aidha kupitia incubators, kampuni zinazokuwa katika incubator husika hukua kwa ukaribu na kutengeneza mahusiano yenye faida katika biashara zao na mitandao mikubwa hata baada ya kuachana na incubator hiyo pale inapokuwa tayari kufanya operesheni zake kwa uhuru.