Home KILIMO Vijana na kilimo biashara

Vijana na kilimo biashara

0 comment 262 views

Katika kukuza uchumi na kuhakikisha watanzania wanalima kilimo chenye tija, taasisi ya Malembo Farm kupitia programu yake ya Malembo Farm Academy inatoa mafunzo ya kilimo biashara kwa wanafunzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Malembo Farm Lucas Elia anasema “tunawajengea wanafunzi maarifa, uwezo, uelewa na chachu ya dhana kuwa kilimo ni ajira, kwa kuwapa mafunzo ya kilimo biashara wakiwa bado masomoni”.

Anasema kutokana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana kuwa kubwa, wanatoa mafunzo hayo ya kilimo cha mbogamboga kwa mitaji midogo kwa wanafunzi wa shule za sekondari ambapo walianza na shule za Benjamini Mkapa, Msasani Islamic na Tambaza bila malipo.

Anaeleza kuwa “tumekuwa tukifanya mafunzo ya kilimo na ufugaji kwa vijana na wajasiriamali wadogo ili kuwapa maarifa na taarifa zitakazo wasaidia kujikita moja kwa moja katika shughuli za kilimo cha kisasa”.

Elias anasema “takwimu zinaonesha kila mwaka vijana laki 8 wanaingia katika soko la ajira lakini ni asilimia 10 pekee wana uhakika wa kupata ajira, ndio maana tumeona ni vema kuwapa mafunzo ya kilimo vijana ili waweze hata kujiajiri katika sekta hii”.

Kupitia kalenda yao ya mwaka, wana programu mbili tofauti ikiwemo ya Ndoto yangu university tour ambapo wanatoa mafunzo kilimo biashara kwa wanafunzi kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Dar es Salaam ikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), DUCE, ARDHI, IFM, na chuo cha Mwalimu Nyerere ambapo takribani wanafunzi 50 wapo kwenye mafunzo.

Anasema programu nyingine ni Agricultural training. “Programu zote hizi mbili ziko chini ya mkakati wa Malembo Farm Academy na zimepangwa kufanyika kwa kipindi cha mwaka mzima na kwa kuanza tulianza na mkakati wa mafunzo ya kilimo kwa wanafunzi wa shule za msingi, vyuo vikuu na shule za sekondari za jijini Dar es salaam bila gharama yoyote ile”.

Elias anafafanua kuwa mkakati huu uliandaliwa na taasisi na ulianza utekelezaji wake mnamo mwezi wa tatu mwaka 2020 kwa dhumuni kubwa la kuwajengea uwezo wanafunzi katika eneo la taarifa muhimu na maarifa yatakayo wawezesha kuwekeza lakini pia kufanya shughuli mbalimbali za kilimo ili kupunguza tatizo la ajira kwa vijana nchini.

Mchakato huu ulifanyika ili kuongeza uelewa na chachu ya dhana ya kilimo ni ajira kwa vijana. Mpango mkakati huu ulijikita zaidi katika kuhakikisha vijana walioko mashuleni lakini pia vyuoni wanajengewa uwezo wa kufanya kilimo ingali bado wakiwa masomoni ili kusaidia kupunguza sintofahamu ya nini watafanya baada ya kumaliza masomo yao.

“Mafunzo yetu ni endelevu ambayo yamegawanywa katika sehemu kuu tatu ikihusisha kipindi ambacho wanafunzi wanapewa mafunzo kwa nadharia, pia kipindi ambacho wanafunzi wanapelekwa katika maeneo ya mashamba ili kuona jinsi kilimo kinafanyika pamoja na maeneo ya viwanda vya kuongeza thamani, na hatua ya mwisho ni kufanya mradi wa kilimo (kilimo cha bustani) ambao unakuwa chini ya usimamizi wa taasisi ili wanafunzi waweze kupata uhalisia wa shughuli za kilimo kwa kuziona changamoto na namna ya kuzitatua” anaeleza Elias.

Soma:

Ukosefu wa ajira kwa wahitimu elimu ya juu bado changamoto

Vijana tumieni mitandao ya kijamii kukuza uchumi

 

Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania ina hekta milioni 44 zinazofaa kwa kilimo cha biashara lakini ni asilimia 10 pekee inayotumika kwa kilimo biashara huku asilimia 90 ikitumiwa na wakulima wadogo na wa kati.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter