Na Mwandishi wetu
Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) imetangaza kutekeleza miradi mbalimbali ya maji na uondoaji wa majitaka katika jiji la Dar es salaam na baadhi ya maeneo katika mkoa wa Pwani ili kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo mbalimbali pamoja na kukusanya na kusafisha majitaka. Mamlaka hiyo inakadiriwa kutoa huduma kwa watu takribani milioni 5.9 katika jiji la Dar es salaam na miji ya Bagamoyo na Kibaha.
Ili kuboresha huduma ya majisafi jijini Dar es salaam, DAWASA imekamilisha miradi ya upanuzi wa mtambo wa maji wa Ruvu Chini pamoja na ule wa Ruvu Juu. Pia ili huduma ya maji iwafikie wananchi wengi zaidi, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na mamlaka hiyo inatekeleza mradi wa kuboresha mfumo wa upatikanaji maji jijini na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani, lengo kubwa likiwa kurahisisha upatikanaji wa maji kwa wenye viwanda, biashara na hata wananchi wa kawaida.
Mbali na hayo mamlaka hiyo imeanza kutekeleza miradi itakayokusanya na kuondoa majitaka ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo mitatu mikubwa na ya kisasa kwa ajili ya kusafisha majitaka.