Na Mwandishi wetu
Baada ya kukamilisha hatua za awali za utekelezaji, serikali leo hii itatangaza rasmi zabuni kwa wakandarasi wa ndani na nje ya nchi ili wapate kuomba kazi ya kutekeleza mradi wa Stieglers Gorge. Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuanza ndani ya kipindi cha miezi miwili ijayo mara baada ya taratibu za zabuni kukamilika.
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dk. Medard Kalemani jijini Dar es salaam ambaye alisema kuwa mkandarasi atakayepewa kazi hiyo anapaswa kuridhia kujenga kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi. Naibu Waziri huyo pia aliongeza kuwa wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi wameshakutana na kuchagua sehemu za kujenga mradi huo katika Mto Rufiji.
Hivi sasa Shirika la Umeme (TANESCO) limeanza upembuzi yakinifu ya kujenga miundombinu itakayopeleka umeme huku Wakala wa barabara (Tanroad) wakishughukilia ujenzi wa barabara ya kufika mahali mradi huu utakapojengwa.