Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla amepiga marufuku ufanyaji wa biashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara zote za Mkoa huo baada ya utaratibu huo kuwa chanzo cha uvunjifu wa amani na ongezeko la ajali.
RC Makalla ametoa maelekezo hayo alipotembelea soko la Kariakoo na kujionea kero ya ufanyaji biashara holela kwenye maeneo ya njia za watembea kwa miguu.
Kutokana na hilo RC Makalla amewaelekeza Mkuu wa Wilaya ya Ilala kufanya kikao na wafanyabiashara hao Jumatatu ya September 13 na kuainisha maeneo ya kuwapeleka waliovamia hifadhi ya barabara.
Aidha, RC Makalla amewaelekeza kuangalia utaratibu mzuri wa kufunga na kufungua baadhi ya Mitaa Kariakoo kwaajili ya kupata maeneo ya kufanya biashara kutokana na ufinyuili wafanyabiashara wote waweze kupata riziki.
Hata hivyo amesema kwa tathimini aliyofanya amebaini hali ya ufanyaji biashara holela Dar es Salaam ipo kwa kiwango kikubwa na kuwanyima watembea miguu haki zao za msingi.
Pamoja na hayo RC Makalla ameelekeza Manispaa zote za Mkoa huo kuweka vibao vya kuzuia biashara kwenye maeneo ya watembea kwa miguu.
Wamachinga wamekiri kuingilia maeneo ya watembea kwa miguu na kuahidi kuhama.