Home BIASHARA Mshikamano kuongeza kasi ya ukuaji uchumi

Mshikamano kuongeza kasi ya ukuaji uchumi

0 comment 107 views

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kudumisha amani, umoja, mshikamano na Muungano, ili kuendelea kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa.

Rais Samia amesema mambo hayo yatafanya mageuzi ya kiuchumi kila inapolazimu kuendana na kasi ya uchumi wa dunia.

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika, Rais Samia amezungumzia maswala mbalimbali ya maendeleo baada ya taifa kupata uhuru wake Disemba 9, 1961 kutoka kwa Mwingireza.

Amesema Uhuru wa Tanganyika ulikuwa chachu na mchango muhimu katika kuwezesha mapinduzi matukufu ya Zanzibar Januari 12, 1964.

Akizungumzia suala la uchumi, amesema dira ya maendeleo ya mwaka 2025 inaelekea kumalizika huku uchumi wa nchi unatarajiwa kukua kwa asilimia 8.

“Tunapoangalia mbele, tunakwenda kuandaa dira ya miaka 25 ijayo ambayo itatutoa mwaka 2025 hadi mwaka 2050, itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla kwa kutoa kipaumbele sekta zinazogusa wananchi moja kwa moja,” amesema.

Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, Rais Samia amesema vimeendelea kuwa huru na hadi sasa magazeti na majarida yaliyosajiliwa nchini yamefikia 270, redio 198, redio za mtandaoni zaidi ya 200, blog 120, televisheni 51, televisheni za mtandao zaidi ya 500 ikilinganishwa na chombo kimoja wakati wa uhuru.

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kutunza mazingira na kuyalinda kwa wivu mkubwa ili kurithisha vizazi vijavyo nchi yenye neema kama ilivyopokelewa kwa vizazi vilivyotangulia.

Viongozi kutoka nchi mbalimbali walihudhuria maadhimisho hayo ambapo Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta alikuwa mgeni rasmi.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter