Home BIASHARAUWEKEZAJI Mteja ni mfalme: Waziri wa utalii

Mteja ni mfalme: Waziri wa utalii

0 comment 119 views

Serikali ya Tanzania imesema itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa sekta ya utalii pamoja na kuendelea kuboresha  huduma za kitalii.

Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa leseni ya shughuli za utalii kwa uharaka zaidi na mifumo ya malazi.

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk Damas Ndumbaro amesema hayo jijini Dares Salaam wakati akikabidhi vyeti kwa wawekezaji waliokidhi vigezo na  kufanikiwa kupata maeneo ya uwekezaji mahiri katika maeneo ya wanyamapori (SWICA) yanayosimamiwa na  Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) ambao ni kampuni  za  Grumet  Services Ltd na Mwiba Holding LTD.

Dk Ndumbaro amesema Wizara ya Maliasili na Utalii itaendelea kutoa fursa katika maeneo yaliyohifadhiwa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi.

Amewasisitiza wawekezaji wazawa pamoja na wa kigeni kulinda na kutangaza utalii na maeneo ya uhifadhi na vivutio hapa nchini, katika maeneo waliyopewa kuwekeza kwa kushirikiana na Serikali.

Pia Waziri Ndumbaro ametumia fursa hiyo kuwahamasisha wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini, akiitaja Tanzania kuwa ni salama, yenye amani na demokrasia na kwamba Wizara anayoiongoza imefungua milango kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini.

“Sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii, falsafa yetu ni moja tu, mteja ni mfalme. Ndio maana mimi, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, tuko tayari kukutana na mwekezaji wa aina yoyote yule, muda wowote ule kujadili changamoto zozote zile, milango iko wazi,” amesema.

Ameipongeza Tawa kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kulinda na kuhifadhi rasilimali za Taifa akisema kuwa Taasisi hiyo ni changa kuliko Taasisi zingine lakini wanafanya kazi ngumu na mazingira magumu zaidi ila wanafanya vizuri.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi Tawa, Meja Jenerali mstaafu Hamis Semfuko, ameishukuru Serikali kwa kuipatia Tawa Sh12.9 bilioni ili kutekeleza miradi ya miundombinu ya utalii kupitia kampeni ya Maendeleo ya Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya Uviko-19.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter