Dola za Kimarekani milioni 15 sawa na Tsh. bilioni 34.5 zitatolewa kusaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya Uzazi ,Mama na Mtoto kwa kipindi cha miaka mitatu.
Msaada huo unatolewa na Taasisi ya Suzan Thompson Buffet Foundation (STBF) yenye Makao Makuu yake nchini Marekani.
Hayo yamebainishwa katika mazungumzo baina ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na Mtendaji wa taasisi hiyo Prof. Senait Fisseha katika kikao cha 14 cha Wafadhili wa Afya ya Mama, Mtoto na Vijana (Global Financing Facility for Women Children and Adolescent Health) Jijini Paris.
Waziri Ummy amesema fedha hizo zitasaidia kuimarisha utoaji wa huduma za afya ya uzazi ikiwemo kuhakikisha kuwa watoa huduma wa afya ngazi ya msingi ya jamii wanapatikana wakutosha.
Aidha, Waziri Ummy amemshukuru Prof. Senait na kuahidi kuwa fedha hizo zitasimamiwa kikamilifu ili kuleta matokeo yaliyokusudiwa ya kuokoa maisha ya wanawake, watoto na vijana.
Ameongeza kuwa fedha hizo zitaelekezwa kuimarisha utoaji wa huduma kwenye vituo vya kutolea huduma ikiwemo huduma rafiki kwa vijana.
Naye, Prof. Senait amesema ameiona dhamira njema ya Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuimarisha huduma za afya ya Uzazi, Mama na Mtoto hivyo wapo tayari kumuunga mkono ili aweze kutimiza vyema maono yake.
Taasisi ya STBF imeonesha nia ya kuongeza fedha zaidi kwa Tanzania endapo utekelezaji wa msaada huo utakuwa wa mafanikio.