Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Sensa ya Majengo kuanza kesho Agosti 30

Sensa ya Majengo kuanza kesho Agosti 30

0 comment 191 views

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi 2022, Anne Makinda amesema sensa ya majengo nchini itaanza kesho Jumanne Agosti 30, 2022 na itafanyika kwa siku tatu.

Makinda amesema hayo jijini Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya Sensa ya Watu na Makazi ambapo ameeleza kuwa asilimia 93.45 ya kaya zote Tanzania zimehesabiwa hadi kufikia leo Jumatatu Agosti 29, 2022 saa 2 asubuhi.

“Kama mnavyofahamu Serikali imepanga pia kufanya Sensa ya Majengo mara tu baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu. Sensa hii itajumuisha kukusanya taarifa za majengo yote ya makazi na yasiyo ya makazi nchi nzima kwa ajili ya kuboresha Sera na kupanga mipango ya kimkakati ya kuboresha sekta ya nyumba nchini,” ameeleza Makinda.

Amebainisha kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku tatu kuanzia Agosti 30, 2022 hadi Septemba 1, 2022.

“Napenda kutoa wito kwa wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa makarani waliowahesabu katika maeneo yenu kwa kutoa taarifa sahihi za majengo” amesema Makinda.

Amesema sensa hiyo ya majengo itafanywa na makarani waliofanya Sensa ya Watu na Makazi ambao watapita kwenye majengo yote yaliopo kwenye maeneo ya kuhesabia watu ili kukusanya taarifa za majengo.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter