Home BIASHARA Bashungwa aingilia kati malalamiko stendi ya Magufuli

Bashungwa aingilia kati malalamiko stendi ya Magufuli

0 comment 185 views

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Amos Makalla  kukutana na wadau na wamiliki wa mabasi ili kuweka utaratibu mzuri ambao ni shirikishi wa utoaji huduma  kwenye Kituo Kikuu cha mabasi cha Magufuli Dar es salaam.

Bashugwa ametoa maelekezo hayo Agosti, 30, 2022 wakati akitoa ufafanuzi kuhusu malalamiko ya utoaji wa huduma kwa wananchi wanaoingia Mkoa wa Dar es salaam kupitia kituo kikuu cha Mabasi cha Magufuli.

Bashungwa amesema amekuwa akifuatilia kwa ukaribu malalamiko yanayotolewa na wananchi kuhusu huduma zinazotolewa katika stendi ya Magufuli kwa abiria wanaoingia na kutoka katika mkoa wa Dar es salaam ambayo yanatafsiri vibaya malengo ya Serikali ya kutenga bilioni 50 kujenga stendi hiyo.

“Kuna abiria wanaoingia Dar es salaam na kushushwa katika stendi ya Magufuli lakini wanahitaji mabasi hayo yawafikishe mjini  kwenye vituo vya mabasi vilivyojengwa na sekta binafsi, kwahiyo Mkuu wa Mkoa akikuta na wadau hao wataona namna nzuri ya kusimamia suala hilo,” amesema Bashungwa.

Aidha, amemtaka Mkuu wa Mkoa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na wadau wengine ili kukubaliana na kuweka utaratibu utakaorahisisha utoaji wa huduma bora bila kuleta adha kwa wananchi wala kuathiri malengo ya Serikali kujenga stendi hiyo.

Amesema Serikali inaweza kutimiza malengo na kusudi la uwepo wa Stendi ya Magufuli bila kuwapa adha wananchi wanaolazimika kushushwa katika stendi na kuingia kwenye gharama za  kutafuta usafiri mwingine wa kuwafikisha mjini wakati yapo mabasi yanaweza kupita katika stendi na yakaendelea na safari ya kuwafikisha abiria mjini.

Amefafanua kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wananchi na kuendelea kuimarisha usalama wa wananchi na wageni wanaoingia nchini kwa kutumia usafiri wa magari kwa kuwatambua kupitia stendi hiyo ambayo kuna idara ya Uhamiaji na vyombo vingine vya usalama.

Hivi karibuni baadhi ya abiria waliokuwa wakisafiri kutoka Arusha na Moshi kuja jijini Dar es Salaam waligoma kushuka katika stendi ya Magufuli.

Kumekuwa na malalamiko juu ya abiria kulazimishwa kushuka katika kituo hicho ilihali mabasi hayo huendelea na safari ambapo mengine huelekea mjini ambapo kuna vituo vyao binafsi huku mengine yakiende nje ya mji.

Wananchi wamekuwa wakilalamika kushushwa katika stendi hiyo na kuanza kutafuta usafiri mwingine wa kuwafikisha mjini na maeneo mbalimbali ambapo gharama zake ni kubwa.

“Mimi ninaenda Sinza, basi hili linafika mpaka Shekilango, hapa nina mizigo mingi, ukiniambia nishuke hapa nitafute usafiri mwingine hadi Sinza sio chini ya 20,000 wakati nikishuka pale Shekilango usafiri ni 2,000 mpaka nyumbani,” anasema mmoja wa abiria.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter