Takribani Taasisi 50 zinatarajiwa kushiriki Kongamano la Biashara la Kimataifa lililoandaliwa na Jukwaa lijulikanalo kama ‘China Trade Week’ (CTW) na kuwahusisha wafanyabiashara mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.
Kongamano hilo litakalohusisha maonesho zaidi ya bidhaa 200, litafanyika Septemba 26 hadi 28 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee.
Bidhaa hizo ni pamoja na bidhaa za kielektroniki, afya, viwanda, mavazi, urembo na ujenzi.
Kwa mujibu wa waandaaji wa kongamano hilo, Zahor Ahmed, amesema tukio hilo linalofanyika kwa mara ya kwanza nchini pamoja na mambo mengine limelenga kuendelea kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na China.
“Kongamano hili limelenga kufungua uchumi wa kimataifa kwa mataifa haya mawili na dunia nzima, biashara itakuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo taifa,” ameeleza Ahmed.
Amebainisha kuwa kongamano hilo ambalo Tanzania itakuwa taifa la sita kuwa mwenyeji limeshafanyika katika nchi za Kenya, Ethiopia, Afrika Kusini, Ghana na Morocco yakijumuisha maonesho ya bidhaa mbalimbali.
Mbali na faida za kiuchumi, kongamano hilo pia litasaidia uwekezaji na kubadilishana tamaduni zilizohusu sekta za ujenzi wa miundombinu, nishati, kilimo, chakula, sayansi na teknolojia.