Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imetakiwa kutumia weledi wake kufanya tafiti na kuja na matokeo ya tafiti hizo kwa wakati ili Wizara iweze kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya wanyamapori nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema hayo Jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWIRI, Dkt. David Manyanza.
Amesema TAWIRI ni injini ya uhifadhi nchini hivyo inapaswa kuwajibika ipasavyo ili iweze kutoa matokeo na majibu ya changamoto zinazoikabili sekta ya wanyamapori nchini.
Amesema matokeo ya tafiti za sensa ya wanyamapori ambazo zimekuwa zikifanywa na TAWIRI zimekuwa zikitoa dira na mwelekeo sekta ya wanyamapori nchini kujitazama iwapo inafanya vizuri na mahali gani juhudi ziongezwe ili wanyamapori waendelee kuwepo.
Amesema Tawiri lazima ifanye tafiti na kutoa majibu kwa wakati kwa kuwa ni Taasisi inayoonesha viashiria hatarishi kwa ustawi wa wanyamapori nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), Dkt. David Manyanza amemhakikishia Waziri kuwa katika kipindi chake cha uongozi moja ya kipaumbele chake ni kufanya tafiti kwa muda na kutoa matokeo ya tafiti hizo kwa muda ili Watanzania waendelee kunufaika na taasisi hiyo.
“Moja ya vitu tunavyojivunia ni kuwa na timu nzuri ya wataalam wenye ushirikiano, nakuhakikishia tafiti tutakazozifanya zitazingatia weledi na kutolewa kwa muda muafaka”.