Home BIASHARAUWEKEZAJI Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji: Mwigulu

Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji: Mwigulu

0 comment 130 views

Serikali kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo wamefanya majadiliano ya uboreshaji mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini illi kuwavutia wawekezaji.

Hayo yamelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba wakati akifungua Mkutano wa ngazi ya juu wa Majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Serikali imesema itaendelea kuwekeza nguvu kwenye maeneo yanayohitaji uwezeshwaji fedha kama vile kilimo, uvuvi na mifugo ili kukuza uchumi, ajira na maendeleo ya jamii.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi na kutoa wito kwa wawekezaji wote kuja kuwekeza nchini na kutumia fursa zilizopo kupata faida yao na nchi kwa ujumla.

“Miaka kadhaa iliyopita kulikuwa na malalamiko ya wafanyabiashara kuhusu utitiri wa kodi, Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarakani alifuta tozo na kodi zaidi ya 114, katika sekta za uzalishaji,”, amesema Dkt. Nchemba.

Amesema moja ya hatua ambazo Serikali ya awamu ya sita imechukua ni kurekebisha sheria za kikodi na sheria za uwekezaji ili kuwepo na mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini.

Dkt. Nchemba amesema kuwepo kwa ushirikiano kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo kumewezesha ufanisi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Washirika hao wa Maendeleo wamekuwa wakiifadhili.

“Tulisaini makubaliano kwenye ziara ya Rais Samia nchini China kuhusu samaki, parachichi, kwenye ziara yake ya Ulaya makubaliano yalisainiwa katika masuala ya nafaka ambapo mchele wa Tanzania unauzwa mpaka Ubelgiji, pia tulisaini na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na nchi nyingine zinazotuzunguka,”ameeleza Dkt. Mwigulu.

Kuhusu uzalishaji katika kilimo, mifugo na uvuvi, amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 mchango wa sekta hizo uwe umezidi asilimia 10 ili Pato la Taifa linapopanda na pato la mtu mmoja mmoja nalo lipande.
Amesema mpaka sasa vijana zaidi ya 27,000 wamejiandikisha kwa ajili ya kutaka kwenda kuwekeza kwenye mashamba maalumu ambayo serikali imepanga vijana wawekeze.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter