Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imetangaza fursa za kuuza bidhaa za vyakula katika soko la Saudi Arabia na nchi za Ghuba.
Uuzaji wa bidhaa hizo unafanyika kwa njia ya soko mtandao wa Kampuni ya Saudi Arabia ya FOODI.
Taarifa ya TanTrade kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia inataja bidhaa hizo kuwa ni pamoja na matunda yaiyokaushwa, kahawa, chai, korosho, viungo, asali, mbogamboga pamoja na vyakula vingine.
“Bidhaa hizo zinatakiwa kukidhi ubora wa kimataifa (content&package) pamoja na viwango vinavyokubalika katika soko hilo,” imesema taarifa hiyo.
Mfumo wa soko hilo umesajili wasambazaji na wanunuzi wa vyakula wapatao 2,000 wakiwemo wamiliki na waendeshaji hoteli na migahwa na zaidi ya aina 14,000 za bidhaa za vyakula.
“Kufuatia taarifa hiyo, kampuni mbalimbali za Tanzania zenye nia ya kuuza na kutangaza bidhaa mbalimbali za vyakula katika soko hilo zinatakiwa kuwasilisha taarifa za bidhaa inayokusudiwa kuuzwa kwa kujaza fomu iliyopo katika tovuti TanTrade,” imeeleza taarifa hiyo.