Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Wajumbe Dira ya Taifa ya Maendeleo wanolewa

Wajumbe Dira ya Taifa ya Maendeleo wanolewa

0 comment 151 views

Serikali imeanza kutoa mafunzo kwa wajumbe wa Timu Kuu za Uandishi na Uhariri wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ili kuhakikisha zinakuwa na uelewa wa pamoja kuhusu machakato wa maandalizi ya Dira hiyo.

Warsha hiyo elekezi ya siku nne inafanyika katika ukumbi wa PSSSF Golden Jubilee Tower, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika ufunguzi wa warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Lawrence Mafuru amesema kuwa warsha hiyo ni msingi madhubuti wa kufanikisha maandalizi ya Dira mpya Taifa ya Maendeleo.

“Matumaini yangu kwamba kupitia warsha hii mtapata muda mzuri wa kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujadili kwa kina kuhusu maono ya Taifa letu kwa kizazi cha sasa na kijacho”, amesema Mafuru.

Amesema anaamini kuwa mafunzo hayo yatawawezesha kutekeleza majukumu yao kakimilifu na kutoa mawazo mazuri kwa kujifunza kupitia Dira za nchi zinazoendelea na zilizoendelea kwa kuwianisha na mazingira ya Tanzania.

Ameongeza kuwa maandalizi ya Dira 2050 yameanza mapema ikizingatiwa kuwa Dira tunayoendelea kuitekeleza kupitia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 itafika ukomo mwaka 2025.

Amebainisha kuwa maandalizi ya Dira yanajumuisha hatua na shughuli nyingi ambazo zinahitaji muda mwingi hivyo zoezi hilo linapaswa kufanywa haraka na kwa kuzingatia muongozo na mpango kazi wa maandalizi ya Dira ili kufikia lengo lililokusudiwa.
Mafuru amewasihi wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa ubunifu, weledi na kujituma kwa kuzingatia hadidu za rejea zilizoandaliwa.

“Nasisitiza utendaji kazi wa majukumu yenu ufanyike kwa ushirikiano ili kutengeneza timu bora na ya ushindi, mara zote jumuiya au jamii isiyo na umoja huishia kwenye migogoro na mifarakano”, ameongeza Mafuru.

Wizara ya Fedha na Mipango inaendelea na taratibu mbalimbali za Maandalizi ya Dira mpya ya Maendeleo ya Taifa 2050 itakayoleta maono ya watanzania kwa miaka 25 ijayo kwa kushirikisha wadau wote muhimu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter