Serikali imesema kuwa inatoa msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa forodha kwenye vifaa vilivyotengenezwa mahususi kwa ajili ya watu wenye mahitaji maalum.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Hamad Hassan Chande (Mb) alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Grace Victor Tendega aliyetaka kujua utayari wa Serikali kuondoa kodi kwenye vifaa vinavyotumiwa na watu wenye ulemavu wakati wa kuingia nchini.
Chande amesema msamaha wa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) umeainishwa katika kipengele cha nane (8) na 12 (d) cha Jedwali lililopo kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, SURA 148.
“Vifaa vilivyopewa msamaha wa kodi ni pamoja na baiskeli na magari yaliyotengenezwa mahususi kwa matumizi ya Watu Wenye Ulemavu”, amebainisha Naibu Waziri.
Ameongeza kuwa Serikali inatoa msamaha wa VAT kwenye huduma za elimu zinazotolewa katika vituo vya mafunzo ya mwili na akili kwa watu wenye mahitaji maalum.