Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Tanzania yaongoza kwa Simba, Nyati na Chui barani Afrika

Tanzania yaongoza kwa Simba, Nyati na Chui barani Afrika

0 comment 207 views

Tanzania inaongoza kwa kuwa na Simba, Nyati na Chui wengi katika bara la Afrika huku ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na idadi kubwa yaTembo.

Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Kairuki amesema hayo April 22, 2024 wakati akitangaza rasmi matokeo ya Sensa ya Wanyamapori na kuzindua taarifa ya Watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023.

Sensa hiyo ya wanyamapori imefanywa na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamaori (TAWIRI) kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Idara ya Wanyamapori, na Frankfurt Zoological Society katika mifumo ya ikolojia ya Nyerere-Selous-Mikumi, Saadani-Wamimbiki na Serengeti.

Mkutano huo uliwahusisha wadau wa uhifadhi na utalii, ambapo Kairuki amesema tayari Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya sensa ya wanyamapori nchi nzima mapema hapo mwakani.

Aidha, amesema matokeo ya sensa hiyo yatasaidia kwenye usimamizi wa wanyamapori nchini na kupanga mipango mbalimbali ya kuboresha uhifadhi na kutangaza utalii duniani.

Waziri Kairuki ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana na Serikali ambapo ameitaka TAWIRI kuandaa mpango kazi kwa ajili ya sensa ijayo huku pia akielekeza watendaji wa wizara yake kuchambua kwa kina matokeo ya sensa hii ili yaweze kuleta tija.

Akitoa taarifa ya sensa hiyo amesema spishi zilizoonesha idadi kubwa ni pamoja na Nyati (59,878), Tembo (20,006), Nyumbu (19,060), Kongoni (18,361), swalapala (14,031) na Ngiri (13,806).

Amezitaja spishi zilizoonesha idadi ndogo ni pamoja na Twiga (1,679), Tandala mkubwa/ kudu (1,414) na puku/sheshe (496).

Amefafanua kuwa kwa upande wa Tembo, idadi imeongezeka kutoka 15,501 mwaka 2018 hadi 20,006 mwaka 2022.

Amebainisha kuwa viashiria vya ujangili wa tembo au vifo vya tembo vimepungua kwa kiasi kikubwa hadi 0.8% mwaka 2022 ikilinganishwa na 16% wakati wa sensa ya 2018.

Akizungumzia kuhusu taarifa ya watalii wa Kimataifa walioitembelea Tanzania mwaka 2023 amesema Sekta ya Utalii imeendelea kuimarika baada kuathiriwa na mlipuko wa janga la UVIKO-19.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter