Home BIASHARA Serikali: hatujazuia biashara mazao ya misitu

Serikali: hatujazuia biashara mazao ya misitu

0 comment 186 views

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema haijazuia biashara ya mazao ya misitu.

Imewataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu kufuata Sheria, Kanuni na Taratibu zilizowekwa ili kuhakikisha kuna kuwa na usawa katika biashara hiyo pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali hiyo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja (Mb) ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kibaha vijijini Michael Costantino Mwakamo, aliyetaka kujua kauli ya serikali juu ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu wanaozuiwa kufanya biashara na Wakala ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

”Natoa rai kwa wafanyabiashara wote wenye nia njema ya kuvuna au kufanya biashara ya mazao ya misitu wafuate Sheria, Kanuni na taratibu zilizowekwa” amesisitiza Masanja.

Amesema Sheria ya Misitu Sura ya 323 na Kanuni zake za mwaka 2004 zimeelekeza utaratibu unaopaswa kufuatwa ili kuvuna, kusafirisha na kuuza mazao ya misitu kwa kuzingatia umiliki wa misitu/miti ambao ni ya watu binafsi, Serikali za vijiji, Serikali za mitaa au Serikali Kuu.

Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Agnes Mathew Marwa, kuhusu Serikali kuwatafutia eneo mbadala Wananchi wa vijiji vya Kata ya Nyantwari – Bunda wanaofanyiwa uthamini kupitisha uhifadhi Masanja amesema kuwa zoezi la uthamini lipo katika hatua za mwisho na baada ya hapo wananchi watalipwa fidia kwa mujibu wa sheria itakayohusisha gharama za thamani ya ardhi, mazao, majengo, posho ya kujikimu, usafiri na posho ya usumbufu.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda imetenga na kupima viwanja 350 katika eneo la Virian-Kata ya Stoo ambapo wananchi watakaohama kutoka Kata ya Nyantwari watapewa kipaumbele wakati wa uuzaji wa viwanja hivyo.

Aidha, Halmashauri ya Mji wa Bunda imeandaa mpango wa kutwaa na kulipa fidia maeneo mbadala ya makazi yenye ukubwa wa ekari 1,625 katika maeneo ya Manyamanyama/Bitaraguru; Butakale; na Guta/Nyabehu.

Maeneo yote hayo yatapimwa na kupewa kipaumbele kwa wananchi wanaotoka Kata ya Nyantwari.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter