Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa kanuni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni za mwaka 2023 ambazo zimeweka madaraja matatu ya leseni za biashara ya kubadilisha fedha za kigeni nchini.
Taarifa ya BoT inasema imeweka madaraja hayo ambayo ni daraja A, B na C chini ya Sheria ya Fedha za Kigeni (Sura namba 271).
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema kwa duka la kubadilisha fedha za kigeni daraja A, ni duka linalomilikiwa na wageni au wenyeji lililoruhusiwa kufungua matawi sehemu yoyote ndani ya nchi.
Ameeleza kuwa duka hilo kama linamilikiwa na wageni litatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Tsh bilioni moja na Tsh milioni mia tano kwa wenyeji.
Amebainisha kuwa duka hilo litaruhusiwa kufanya miamala papo kwa hapo, kutuma fedha na kufanya biashara kama wakala wa benki, taasisi ya fedha, kampuni ya bima, mtoa huduma kwa njia ya simu, au huduma nyingine zozote za fedha kama itakavyoidhinishwa na BoT.
Kwa upande wa daraja B amesema ni duka linalomilikiwa na wenyeji na halitaruhusiwa kufungua matawi na litatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Tsh milioni mia mbili.
Ameeleza kuwa duka hilo litaruhusiwa kufanya miamala ya papo kwa hapo na kufanya biashara kama wakala wa benki, taasisi ya fedha, kampuni ya bima, mtoa huduma wa fedha kwa njia ya simu, au huduma nyingine zozote za fedha kama itakavyoidhinishwa na BoT.
Gavana Tutuba ameeleza daraja C kuwa ni duka lililoanzishwa na hoteli yenye hadhi ya nyota tatu au zaidi kwa ajili ya kufanya miamala ya papo kwa hapo kwa wateja wa hoteli pekee.
Amesema leseni hiyo itatolewa kwa hoteli husika au mmiliki wake na kuwa haitatakiwa kuwa na mtaji wa kufanya biashara ya kubadili fedha za kigeni.
Amebainisha kuwa, kanuni hizo za mwaka 2023, zimefuta rasmi kanuni za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni za mwaka 2019.