Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeonyesha utayari wa kuendelea kuimarisha masuala ya uwekezaji, mafunzo na matumizi ya teknolojia katika kukuza sekta ya utalii kwa kufanyia kazi miongozo inayotolewa na Shirika la Utalii Duniani (UNWTO).
Waziri wa Maliasili na Utalii Angellah Jasmine Kairuki amesema hayo baada ya kushiriki Jukwaa la Uwekezaji (Global Investment Forum) lililofanyika sambamba na Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO) unaoendelea jijini Samarkand, Uzbekistan.
Katika mijadala iliyowasilishwa, nchi wanachama zimesisitizwa kuzingatia uwekezaji endelevu unaozingatia utunzaji wa mazingira, kuimarisha uwekezaji katika eneo la mafunzo na matumizi ya teknolojia ili kuendelea kuboresha sekta ya utalii na ukarimu.
Aidha, nchi wanachama zimesisitizwa kuendelea kuboresha miundombinu ili kuvutia watalii wengi zaidi.
Waziri Kairuki pia ametembelea maonesho ya utalii yaliyokuwa yakifanyika sambamba na Jukwaa la Uwekezaji na kujionea vivutio na maendeleo ya utalii nchini Uzbekistan na kushauri wadau wa utalii nchini Uzbekistan kutangaza utalii na bidhaa zao nchini Tanzania ikiwemo kuchangamkia fursa ya maonesho ya kimataifa yanayofanyika nchini Tanzania.
Waziri Kairuki pia amekutana na kufanya mazungumzo na Raximov Jurabek Raximovich, Gavana wa Jimbo la Khorezm, ambalo limepiga hatua kubwa katika utalii wa utamaduni na ubunifu katika kazi za sanaa za mikono (handcrafts).
Kupitia mazungumzo hayo, Kairuki alitoa pendekezo kwa nchi mbili kushirikiana katika kukuza utalii ikiwemo kubadilishana uzoefu katika kukuza utalii wa utamaduni, kuimarisha usafiri wa anga kati ya nchi mbili ili kurahisisha watalii kutembelea nchi zote mbili pamoja na kuimarisha ushirikiano wa wadau wa utalii kutoka sekta binafsi kwa lengo la kukuza utalii.