Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amekutana na wadau wa usafirishaji katika mkutano maalum uliofanyika katika ukumbi wa mikutano Arnatoglo Mnazi mmoja Jijini Dar es Salaam Oktoba 18, 2023 ambapo wadau hao wamewasilisha ombi la kupandishwa kwa nauli.
RC Chalamila amesema wadau wa usafirishaji ni kundi muhimu hakuna anayeweza kubeza ukweli huo, na uwekezaji wowote unaofanywa lazima uwe na tija lakini popote wanapokutana na changamoto njia ya mazungumzo iwe kipaumbele na sio migomo.
RC Chalamila amepata wasaa wa kusikiliza maoni na changamoto zinazoikabili sekta hiyo ambapo kwa sehemu kubwa inatokana na kupanda kwa gharama za mafuta ambapo walio wengi katika mawasilisho yao wameiomba Serikali kupandisha nauli ili waweze kupata faida kuliko hali ilivyo sasa.
Hata hivyo RC Chalamila ameitaka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kukaa pamoja na kujadili kwa kina changamoto hiyo na kuipatia majawabu lakini ni vizuri maamuzi yatakayofanyika yazingatie pia hali halisi ya uchumi wa wananchi.
Amewashuru wadau hao kwa kazi nzuri wanazoendelea kufanya vilevile amemshukuru Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji katika sekta ya usafirishaji na namna anvyoifungua sekta hiyo kwa sasa usafiri upo masaa 24.
Kwa upande wa Baraza la LATRA wamesema Changamoto zinazoikumba sekta ya usafirishaji ni kwa sababu ya kutumia nishati ya mafuta pekee ni wakati muafaka wa kuangalia fursa zingine ikiwemo kuanza kutumia nishati mmbadala ikiwemo gesi katika vyombo vya usafiri kwa kuwa utaalam huo kwa sasa upo hapa nchini.