Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Afrika tujitegemee kifedha mabadiliko tabia ya nchi: Rais Samia

Afrika tujitegemee kifedha mabadiliko tabia ya nchi: Rais Samia

0 comment 170 views

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema ni muda muafaka kwa Afrika kujitegemea katika fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Rais Samia amesema hayo katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) unaojadili Masuala ya Tabianchi na Usalama wa Chakula Mkoani Arusha ulioandaliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

“Tuangalie na tuje na mkakati na mbinu za kuwa na mfuko wetu wenyewe katika kukabiliana na mambo ya mabadiliko ya tabia ya nchi, kwa sababu kutegemea wengine tunachelewesha.

Sasa hivi tupo COP28 lakini ahadi zilitolewa kwenye COP za nyuma huko, lakini mpaka leo fedha haijatoka,” ameeleza Rais Samia.

Mkutano huo unashirikisha Wajumbe wa Baraza la Mawaziri la Kisekta la Jumuiya ya Afrika Mashariki kujadili juu ya Mabadiliko ya Tabia Nchi, Usalama wa Chakula.

Mkutano huo umeshirikisha Mawaziri wa kisekta, wadau mbalimbali wa mazingira na kilimo, kutoka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Ubalozi wa Ujerumani nchini na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ).

Kauli mbiu ya Mkutano huo ni “Kuongeza ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi kwa usalama wa chakula na mazingira endelevu katika ukanda wa Afrika Mashariki”.

Mkutano huo unajadili mada mbalimbali zikiwemo Maazimio ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi wa Nairobi na uwiano wa athari zake kwa eneo la Jumuiya, Maazimio ya Mkutano wa AGRF wa Dar es Salaam kuhusu Usalama wa Chakula na Uwiano wa athari zake kwa eneo la Afrika Mashariki.

Zingine ni kuhakikisha Usalama wa Chakula kupitia mikakati na mbinu mbalimbali za kurekebisha na Kuonesha Mafanikio ya Kilimo cha kisasa kinachotokana na matumizi ya teknolojia na mbinu mbalimbali za ubunifu katika eneo la Afrika Mashariki

Mkutano huo wa Majadiliano ya Juu unatarajiwa kutoa na msimamo wa pamoja wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuelekea Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaotarajiwa kufanyika nchini UAE kuanzia Novemba 28, 2023.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter