Na Mwandishi wetu
Afisa Mtakwimu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar Salma Saleh Ali amesema kuanzia Agosti mwaka huu, mfumuko wa bei wa bidhaa mbalimbali umepanda kwa asilimia 1.4 ambapo bidhaa za chakula na zile zisizo za chakula zimepanda kwa asilimia 6.1 ikilinganishwa na mwezi wa Julai mwaka 2017.
Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Idara ya Kiuchumi za Takwimu Abdul Ramadhani ameshauri wananchi kuwa na mazoea ya kutumia vyakula wanavyozalisha wenyewe kwa wingi huku wakijiwekea utaratibu wa kutunza akiba katika maghala ya chakula ili itumike endapo kutakuwa na upungufu wa chakula. Amesema kufanya hivyo kutasidia kwa kiasi kikubwa kupunguza masuala ya bei kupanda mara kwa mara.
Akitolea maoni juu ya mfumuko wa bei visiwani humo, Mhadhiri wa Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA) Dk. Suleiman Simai Msaraka amedai japo kuwa kumekuwa na ongezeko hilo la bei katika bidhaa mbalimbali, hali siyo mbaya sana kwani mfumuko wa bei upo duniani kote kwahivi sasa nasiyo Zanzibar peke yake.